Na Mwandishi Wetu
MWANAMUZIKI mkongwe nchini Roy Mukuna (kulia) amefariki dunia leo
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, imeelezwa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kiongozi wa kundi la
Wazee Sugu, King Kikii, Mukuna alifariki dunia baada ya kulazwa kwa muda katika
hospitali hiyo kutokana na maradhi ya figo na ini.
Mukuna mwenye umri wa miaka 47 wakati wa uhai wake alipitia
katika makundi mbalimbali akipiga zana tofauti tofauti kabla ya kupuliza
saxophone hadi umauti unamkuta.
Msanii huyo hadi anafariki alikuwa kiongozi wa kundi la
muziki wa dansi la Bana Kamanyola ambalo linapiga muziki wake katika klabu ya
Mwanza ya Villa Park iliyopo karibu kabisa na Uwanja wa CCM Kirumba.
King Kikii amesema kuwa kifo cha Mukuna ni pigo kubwa kwani
kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya muziki hapa nchini kutokana na umahiri
wake.
Naye rafiki wa karibu wa Mukuna, Parash Mukumbule amesema leo
kuwa marehemu wakati wa uhai wake alipigia bendi mbalimbali ikiwemo Maquiz,
ambako alitunga kibao cha Scola, Super Tanza, Sendema na Deka Musica.
Anasema kuwa marehemu ameacha mke na watoto watano na mipango
ya mazishi inafanyika nyumbani kwake karibu na mzunguko wa Kigogo jijini Dar es
Salaam.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina.
No comments:
Post a Comment