Rais, Kamati ya Olimpiki Tanzania,Ndugu Gulam
Rashid,
Makamu wa Rais, Kamati ya Olimpiki Tanzania,
Ndugu Henry Tandau
Katibu Mkuu, Kamati ya Olimpiki Tanzania,
Ndugu Filbert Bayi,
Katibu Mkuu, Riadha Tanzania, Ndugu Wilhelm
Gidabuday
Mwakilishi, Chama cha Riadha Zanzibar
Wakufunzi wa Kimataifa, Ndugu Tagara Tendai
na Charles Mukiibi
Waratibu wa Mafunzo, Ndugu Irene Mwasanga
(TOC) na Robert Kalyahe (RT)
Washiriki wa Mafunzo,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Injinia Evarist Ndigilo (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau. |
Napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru ofisi
ya TOC kwa kunipa heshima hii ya kuwa mgeni rasmi katika kufunga mafunzo haya
ya walimu wa mchezo wa Riadha daraja la 1.
Nimefahamishwa kwamba mafunzo haya
yalifunguliwa siku 11 zilizopita na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Mhe. Harrison George Mwakyembe. Ni matumaini yangu kuwa mmepata dozi
nzuri ya taaluma na mbinu mbalimbali ya kufundisha mchezo huu. TOC inauthamini
sana mchezo wa Riadha, kwani ni kati ya
michezo ambayo imeiletea heshima Taifa Taifa letu katika Michezo ya Kimataifa
kama Jumuiya ya Madola, Afrika.
Siwezi kuzungumzia Olimpiki kwani nimefahamishwa tangu tuanze kushiriki
Olimpiki mwaka 1964 mjini Tokyo, Tanzania imewahi kupata medali mbili za fedha
kupitia Filbert Bayi ( Mita 3000 kuruka Magongo) na Suleiman
Nyambui (Mita 5000).
Sote tunakumbuka mwaka 2016 wakati wa Michezo
ya Olimpiki ya Rio, Mtanzania Alphonce Felix Simbu pamoja na kuwa mshindi wa 5
katika mbio za Marathon aliweza kuitoa Tanzania kimasomaso kwa nafasi ambayo
kwa mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1992 mjini Barcelona wakati mkimbiaji wa
Tanzania Kanali Mstaafu Juma Ikangaa alipokuwa wa sita (6) katika mbio za
Marathon.
Kama nilivyofahamishwa haya ni mafunzo ya nne kufanyika kwa walimu wetu
hapa Tanzania. Mafunzo ya awali yalifanyika mjini Dar Es Salaam mwaka 1991,
mjini Dodoma mwaka 2004 na mwaka 2010 mjini Dar Es Salaam na mwaka huu 2017
hapa Mkuza, Kibaha. Mafunzo yote yakifadhiliwa na Olimpiki Solidariti (OS)
kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).
Pia naamini mmefaidika na elimu mliopata
kutoka kwa wataalamu wa Kimataifa ambao wamekuwa wakiwaandalia masomo yote ya
nadharia na vitendo kwa muda wote wa siku 11. Ni mategemeo yangu elimu
mliyopata itawasaidia kuandaa timu zenu na kutambua vipaji vipya katika maeneo
mnayotoka. Ni ukweli usiopingika kwamba mmejiongezea elimu ya kufundisha mchezo
huu wa riadha kwa kiwango cha hali ya juu, mkilinganisha uwezo na elimu
mliyokuwa nayo awali.
Wakati wote TOC imekuwa mstari wa mbele
katika kuendeleza taaluma ya ufundishaji na mbinu za kisasa za kuboresha uwezo
wa walimu wetu, ili wachezaji wetu waweze kufikia viwango vinavyotakiwa na timu
zetu zinaposhindana katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa.
Hivi karibuni tumesikia wanariadha wetu
wakifanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa baada ya Alphonce Felix Simbu
kufungua milango ya ufanisi kwa kuwa wa tano (5) kwenye mbio za masafa marefu
(Marathon) wakati wa Olimpiki ya Rio 2016.
Baada ya mafanikio hayo ya Simbu, kumekuwa na
misafara ya wanariadha wetu kushindana nchi mbalimbali duniani aidha kuongeza
mapato au kufikia viwango vya kushiriki mashindano makubwa ya Dunia
yanayofanyika Augusti, 2017.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ndigilo akimkabidhi cheti, Meta Petro wa Karatu wakati wa hafla hiyo ya kukabidhi vyeti kwa washiriki hao Kibaha. |
Mara kwa mara tumesikia katika mafunzo
yaliyopita walimu wengi wanapohitimu wanakimbilia kufundisha tu michezo ya
kukimbia hususan mbio za masafa marefu
(Marathon) na ndefu (5000/10000) na kusahau michezo mingine, riadha siyo
kukimbia tu, kuna mbio fupi (sprints) kati, (middle distance) kuruka (kuruka
chini, miruko mitatu, kuruka juu na upondo) na kurusha (mkuki, kisahani, tufe
na nyundo).
Ningependa kusisitizia sana kwenu walimu
mnaomaliza mafunzo haya, kwamba
mhakikishe mchezo huu wa riadha
unapiga hatua katika maeneo yote na kufikia viwango vya miaka ya 70.
Tanzania haina tofauti na jirani zetu Kenya
ambao wamekuwa tishio katika mchezo wa riadha duniani.
Ningependa kuwasihi walimu mnaomaliza mafunzo
haya leo kuupeleka mchezo huu mashuleni walipo vijana wengi wenye vipaji vingi
ambao wanafundishika na rahisi kuelewa. Inahitajika mipango mahususi ya mazoezi
na mashindano ambayo nina imani Chama cha Riadha Taifa inayo.
Nyie wachache mliohudhuria hapa muwe mabalozi
wa kupeleka elimu hii kwa wale ambao nao wangependa kuwa hapa, lakini kutokana
na nafasi ndogo ya washiriki kwa maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Riadha
(IAAF) hawakuweza kushiriki.
Kumekwepo na mapungufu ya walimu wa michezo
mbalimbali hasa riadha wakati wa maandalizi ya Umisseta na Umitashumta.
Ninaowaomba kwa kuwa mmetoka karibu kila Mkoa wa nchi yetu (Tanzania
Bara/Zanzibar) muwasaidie walimu hao kabla na mara maandalizi yanapoanza.
Napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza na
kuwashukuru Wataalamu wa Kimatafa kwa jitihada zao za kutoa mafunzo haya kwa
ufanisi mkubwa, waratibu wa RT/ZAAA, TOC na Walimu washiriki kwani bila wao
kuwepo hapa mafunzo haya yasingefanyika.
Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru
Olimpiki Solidariti kwa kufadhili mafunzo haya, Shirikisho la Kimataifa la
Riadha (IAAF) kuwateua Wakufunzi wa kuendesha mafunzo, TOC na RT/ZAAA kwa
maandalizi mazuri, mwisho wenyeji wenu katika Kituo hiki kwa mazingira mazuri
na tulivu kwa mafunzo kama haya.
Mwisho kabisa nawashukuru wale wote
waliohusika katika kufanikisha mafunzo haya kwa namna moja au nyingine.
Kwa haya machache sasa natamka kwamba mafunzo
yenu ya ualimu wa mchezo wa Riadha ninayafunga rasmi na niko tayari kutoa vyeti
mbalimbali.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment