Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania inayoshiriki Michezo ya Sita ya Vijana ya Jumuiya ya Madola, Regina Mpigachai.
|
Na Mwandishi Wetu
MWANARIADHA wa Tanzania Regina Mpigachai ametinga
fainali ya mbio za meta 800 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa vijana
inayoendelea Nassau, Bahamas.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Mpigachai
alipangwa katika kundi la pili la mchujo na alimaliza mbio hizo akiwa katika
nafasi ya tano kwa kutumia dakika 2:11.65.
Kundi la mchujo la mwanariadha huyo lilikuwa na
wachezaji nane na alifuzu kucheza fainali baada ya kuwa mmoja kati ya
wanariadha waliokuwa na muda mzuri zaidi licha ya kutokuwemo katika tatu bora.
Mshindi wa kwanza katika kundi la Mpigachai alikuwa
Anna Lilly aliyetumia dakika 2.11.65 wakati mshindi pili ni Carlet Thomas.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Katibu Mkuu wa
Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema kuwa, Mpigachai kwanza
ameboresha muda wake binafsi mpya baada ya ule wa awali wa dakika 2.13.51
aliouweka katika mashindano ya Kanda ya Tano yaliyofanyika Uwanja wa Taifa.
Bayi aliongeza kusema kuwa mwanariadha huyo pia
pamoja na kumaliza watano, lakini muda wake ulikuwa bora zaidi akiwazidi
wanariadha wote watatu wa kundi la mchujo wa kwanza waliotumia dakika 2.12.21,
2.12.84 na 2.12.86.
Wakati huohuo, mwanariadha mwingine wa Tanzania
Francis Damian alitinga moja kwa moja katika fainali baada ya washiriki wa mbio
hizo kuwa wachache.
No comments:
Post a Comment