DAKAR, Senegal
WATU nane wamekufa na wengine 49 wameumia
baada ya ukuta wa uwanja wa soka kuwaangukia watu nchini Senegal.
Janga hilo lilitokea kwenye Uwanja wa Demba
Diop katika mjini mkuu, Dakar, katika mchezo wa fainali ya Kombe la Ligi kati
ya Stade de Mbour na Union Sportive Ouakam.
Mapigano yalianza kati ya mashabiki wa timu
pinzani na polisi kuingilia kati kwa kutumia mabomu ya machozi, yaliyosababisha
mashabiki kuchanganyikiwa, kukimbia ovyo kukanyagana, na baadae ukuta kuanguka.
Baadhi ya mashabiki walikuwa wakirusha vitu
yakiwemo mawe kwa wenzao na kusababisha vurugu kubwa.
Picha zilizosambazwa katika mitandao ya
kijamii zilionesha watu wakigombea kupanda ukuta, huku wingu la gesi ya machozi
likitanda eneo hilo la uwanja.
Shirika la Habari la hapa (APS) liliripoti
kuwa, magari ya kubeba wagonjwa na yale ya zima moto yalikuwepo katika eneo hilo
la tukio.
Wakati matokeo yakiwa 1-1 baada ya kumalizika
kwa dakika 90, Mbour walifunga katika kipindi cha kwanza cha nyongeza na hatimaye kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, na vurugu kutimka baada ya filimbi ya mwisho.
Cheikh Maba Diop, ambaye rafiki yake alikufa katika tukio hilo na ambaye alisaidia kuondoa watu nje ya
uwanja, aliliambia Shirika la Habari la AFP: “Wakati ukuta ulipoanguka…tulijua
baadhi ya jamaa zetu watakuwa wamepoteza maisha kwa sababu ukuta ule
uliwaangukia watu moja kwa moja.”
Msemaji wa Rais wa nchi Macky Sall alisema
kampeni za Urais zilizokuwa zifanyike leo Jumapili ziliahirishwa ikiwa ni sehemu
ya maombolezo hayo.
No comments:
Post a Comment