WAWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la
Afrika, Simba (Pichani) wameyaaga mashindano ya SportPesa Super Cup baada ya kufungwa na
timu isiyo na jina ya Nakuru All Stars ya Kenya kwa penalti 5-4.
Matokeo hayo ya kufungwa kwa Simba, sasa yanaifanya timu hiyo kuwakwepa
watani zao wa jadi Yanga, ambayo juzi walitinga nusu fainali.
Yanga tayari jana walikaririwa wakisema kuwa wanataka kukutana na Simba
katika fainali ya mashindano hayo ili kuisikisha adabu timu hiyo iliyomaliza ya
pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es
Salaam, timu hizo zilitoka suluhu katika dakika 90 za kawaida na kumsaka
mshindi kwa matuta ili kumpata mshindi.
Mchezaji aliyezamisha jahazi la Simba alikuwa kipa wa timu hiyo, Daniel
Agyei baada ya kukosa penalti ya pili aliyoipiga na hivyo kutolewa kwa 5-4.
Hii ni mechi ya tatu kuamriwa kwa matuta baada ya ile ya Yanga kuitoa
Tusker kwa penalti 4-2, huku Singida United nayo ikitolewa kwa penalti AFC
Leopard kwa penalti 5-4 baada ya kutoka sare ya 1-1 katika dakika 90.
Kwa ushindi huo, Nakuru All Stars iliyopo katika ligi daraja la kwanza
itacheza dhidi ya Wakenya wenzao, Gor Mahia katika mchezo wa nusu fainali
utakaopigwa kesho Alhamisi.
Katika mchezo huo wa Simba na Nakuru, timu zote zilishambuliana kwa zamu
na kukosa nafasi kadhaa za wazi hadi kufikia hatua ya kupigia penalti.
Katika mchezo wa kwanza jana kwenye Uwanja huo, Gor Mahia iliibuka na
ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys ya Zanzibar.
Mabao ya washindi katika mchezo huo yalifungwa na Middie Kagere katika
dakika ya 63 na 83.
Wachezaji wa Simba waliopata penalti ni Mwinyi kazimoto, Hafidh Mussa,
Feston Munezero na Jamvier Bukungu wakati Agyei alikosa.
Wakati penalti za Nakuru All Stars zilifungwa na Nganga Peter, Amakanji
Japheth, Siwa Omond, Maina Geofrey na Nturukundo Jerome.
No comments:
Post a Comment