Na Mwandishi Wetu, Mwanza
UONGOZI wa Mashindano ya Michezo ya Shule za
Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) umeunda Kamati Maalumu kwaajili ya kudhibiti
wanafunzi wenye umri mkubwa ambao wanashiriki katika mashindano hayo.
Akizungumza jijini hapa, Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi
wa Elimu, Jeshi Lupembe alisema wameunda kamati hizo ili kuondoa malalamiko
yanayoletwa na walimu katika mashindano hayo.
Lupembe alisema kamati alizounda zina
watalamu mbalimbali waliobobea katika michezo, ambao hadi sasa uongozi wao
umetoa fomu maluumu kwaajili ya malalamiko yahusuyo wanafunzi waliozidi umri
wanaoshiriki michezo hiyo.
Akielezea zaidi,Lupembe alisema mikoa
inayotuhumiwa kuwa na wachezaji wenye umri mkubwa ni pamoja na Dar es Salaam,
Tanga, Kigoma na Mara.
Lupembe alisema kamati yake kazi kubwa
inayofanya ni kumhoji mtoto husika, kupeleleza mkoa alikotoka, shule, ofisa
elimu, walimu na wazazi kuwahoji ili kujua
umri halali wa mtoto.
Kwa mujibu wa Jeshi, mpaka sasa waliotuhumiwa
katika orodha ya watoto waliozidi umri ni 10 na
katika hao kuna watoto watatu wako vizuri, lakini saba waliobaki
wameonywa kutoshiriki mashindano hayo.
Aidha, Mkurugenzi Lupembe alisema Serikali
itaendelea na jitihada za mazungumzo ya kutafuta udhamini wa mashindano hayo
kama ilivyo kwa Michezo ya Shule za Sekondari (Umisseta).
Katika mechi za leo mpira wa miguu kwa
wavulana, Mwanza imeshinda 3-0 dhidi ya Manyara, Mpira wa mikono wasichana Mara
imeshinda 13-9 dhidi ya Mtwara, Shinyanga 8-5 Dodoma na Mara 6-4 Dar-es-salaam.
No comments:
Post a Comment