Na Mwandishi Wetu
MAAFISA Afya toka kitengo cha magonjwa ya dharura mkoa wa Songwe wameweka
kambi kwenye kiwanja cha ndege cha
Kimataifa cha Songwe (SIA), ili kubaini abiria wenye dalili za ugonjwa wa Ebola
ulioibuka hivi karibuni kwenye nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya
Kongo.
Kiwanja cha Kimataifa cha Songwe kilichojengwa na Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA) mwaka 2012 kinapokea abiria 500,000 kwa mwaka kutoka
sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwemo nchi jirani za Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo. TAA inahudumia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali.
Bi. Shukrani Nkonjeka, Ofisa Afya akimpa maelezo kuhusiana na ugonjwa wa Ebola, mmoja wa wafanyakazi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA), Bw. Fred Martin. |
Ofisa Afya Peter Alfred amesema wamefunga mashine maalum na ya kisasa
kiwanjani hapo, ambayo abiria akipita umbali wa mita tano hadi 10 inampiga
picha na kuonesha joto alilonalo mwilini, na endapo atakuwa na joto la
nyuzijoto 37.5 mashine hiyo itatoa mlio wa kengele.
Alfred amesema abiria atakayekuwa na joto hilo, atachukuliwa na
kupelekwa eneo maalum lililotengwa umbali wa mita 300 kutoka eneo la kiwanja
cha ndege na baadaye kupelekwa hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya
matibabu zaidi.
Hata hivyo, amesema mbali na kuangaliwa kwa abiria wenye joto kali la
mwili, pia hukagua na kupata maelezo binafsi kwa kujaza fomu maalum kwa abiria
wote wanaopita kwenye kiwanja hicho wakitokea kwenye nchi za Kongo, Guinea,
Sierra Leone, Mali, Nigeria, Liberia, Senegal, Marekani na Hispania kutokana na
nchi hizo ziliwahi kukumbwa na ugonjwa huo.
“Hadi sasa tangu zoezi hili
limeanza baada ya kupatikana kwa taarifa za ugonjwa kuwa hapo Kongo, bado
hatujapata mgonjwa mwenye dalili hizo na tunaendelea kuudhibiti kwani hapa ni
njia kuu kwa abiria wanaotoka Kongo ni wengi,” amesema Bw. Alfred.
Alfred amesema ugonjwa wa Ebola unasababishwa na virusi vya Ebola
vinavyoingia mwilini mwa binadamu na wanyama kupitia puani, masikioni na
machoni, na huambukiza kwa kugusa majimaji ya mwili toka kwa mtu aliyeambukiwa
virusi hivyo, yakiwemo matapishi, damu, jasho, mkojo, machozi, kamasi na mate.
Pia binadamu anaweza kupata ugonjwa huu kwa kugusa au kuosha maiti ya
aliyefariki kwa ugonjwa huu au kugusa shuka, godoro, nguo na blanketi
lililotumika na mgonjwa; pia kuchomwa na sindano au vifaa visivyo safi na
salama vilivyotumiwa na mgonjwa wa ebola; au kula matunda yaliyoliwa nusu na
wanyama na kugusa mizoga au kula wanyama pori kama nyani, sokwe na popo.
Amesema dalili za ugonjwa huo zinaanza kujitokeza kati ya siku
mbili hadi 21 baada ya kupata maambukizi, ambapo mgonjwa hupata homa kali ya
ghafla, maumivu ya kichwa, maumivu ya mwili, misuli na viungo, vipele mwilini,
kuvia damu chini ya ngozi, kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni,
kuharisha na kutapika kunakoweza kuambatana na damu.
Hata hivyo, Alfred amesema ugonjwa huu hauna tiba maalum wala chanjo,
lakini mgonjwa hupatiwa tiba saidizi kulingana na dalili alizonazo kama vile
kushusha homa na maumivu, kuongezewa damu na maji mwilini na tiba lishe.
Bi Shukrani Nkonjeka, Afisa Afya akiwapa maelezo yanayohusiana na ugonjwa
hatari wa Ebola madereva wa taxi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe
(SIA).
Alfred amesema wananchi wanaweza kujikinga na ebola kwa kuepuka
kusalimiana kwa kupeana mikono au kukumbatiana, kuepuka kugusa majimaji
yaliyotoka mwilini mwa mgonjwa au kuosha maiti, kuacha kutumia godoro, shuka na
nguo za mgonjwa na pia wawahi haraka kituo cha kutolea huduma za afya endapo
wataona dalili za ugonjwa wa ebola.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA MAHUSIANO, MAMLAKA YA VIWANJA VYA
NDEGE TANZANIA (TAA).
No comments:
Post a Comment