Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya taifa ya riadha yatafanyika
Mkuza, Kibaha mkoani Pwani kwa siku mbili kuanzia Julai 22 na kushirikisha
wanariadha kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm
Gidabuday alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, mashindano hayo awali
yalitakiwa kufanyika mwezi uliopita, lakini yalisogezwa mbele ili kupisha
mashindano ya shule za Sekondari na Msingi ya Umisseta na Umitashumta
inayofanyika Mwanza.
Gidabuday alisema kuwa hatua ya kusoeza mbele
mashindano hayo ya taifa ni kuwezesha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
kushiriki ili kuinua vipaji vyao.
Aliitaka mikoa yote kufanya maandalizi ya
maana ili kueleka timu iliyoiva vizuri kwa ajili ya kutoa ushindani katika
mashindano hayo ya taifa yatakayofanyika kwenye viwanja vya shule za Filbert
Bayi.
Aidha, Gidabuday alisema kuwa benchi la
ufundi la timu ya taifa ya vijana watakaoshiriki mashindano ya dunia kwa
wachezaji wenye umri chini ya miaka 18 limeanguliwa na sasa timu hiyo itakuwa
chini ya kocha mkuu Rehema Killo badala ya Robert Kalihaye.
Alisema kuwa Killo atasaidiwa na Yohana
Misese wakati meneja wa timu hiyo atakuwa Christian Katembo, ambao wanachukua
nafasi ya Mwinga Mwanjala na Peter Mwita. Mwanjala ameteuliwa kuwa kocha wa
wachezaji wa riadha watakaoshiriki mashindano ya Michezo ya Jumuiya ya Madola
ya Vijana itakayofanyika Bahamas baadae mwezi ujao.
Mbali na riadha, Tanzania katika michezo hiyo
ya Madola itashirikisha pia mchezo wa kuogelea ambao nao utakuwa na wachezaji
wawili.
Wakati huohuo, Gidabuday amesema kuwa RT
haihusiki na kuvurundwa kwa mchezo wa riadha katika Michezo ya Shule za
Sekondari nchini (Umisseta) inayoendelea jijini Mwanza, kwani hawakushirikishwa
kwa lolote.
Alisema kuwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT)
liliwatumia barua ya mualiko RT ikiwa imechelewa, hivyo hawajapeleka wataalam
wao katika michezo hiyo, ambayo itafuatiwa na ile ya shule za msingi
(Umitashumta).
No comments:
Post a Comment