Tuesday, 24 October 2017

Naibu Waziri aridhishwa na Ujenzi Terminal Three

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasilian) (kushoto) , Atashasta Nditiye  akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Johannes Munanka wakati alipotembelea kiwanja hicho leo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela. Mwingine ni Ofisa Usalama wa JNIA, Imani Mwakiyarangwe.

 Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye amesema kuwa ameridhika na maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya tatu (Terminal III) ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Nditiye ambaye yuko upande wa sekta ya Uchukuzi na Mawasiliani aliyasema hayo leo baada ya kutembelea sehemu zote za JNIA kuanzia Terminal One hadi Three na kujionea mambo mbalimbali.

Ofisa wa zamu wa Uhamiaji kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Kaanankila Mbise akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa  Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye (kushoto) wakati alipotembelea kiwanja hicho leo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA),  Richard Mayongela.

Amesema kuwa ameridhishwa jinsi ujenzi huo unavyoendelea, ambao unatarajia kukamilika Septemba mwakani.

Amesema kuwa ujenzi unaendelea vizuri tena kwa kasi kubwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto katika mradi huo, ambazo zinafanyiwa kazi.

Alimtaka mkandarasi, ambaye ni Kampuni ya BAM International kuendelea na kazi bila kusita, kwani Serikali imeshatoa fedha za ujenzi huo.

Amesema kuwa pia amefurahishwa na mipango ya biashara baada ya kumalizika kwa kiwanja hicho, ambapo kutakuwa na migahawa, mahoteli jirani na sehemu hiyo ya Terminal Three.

Amesema amegundua changamoto ndogo ndogo kama suala la mpango wa biashara kuwepo na mahoteli kuzungunguka eneo hilo, ambapo tayari amewaagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kushughulikia hilo.

Kingine ni uchakavu wa mashine za kupozea hewa na mashine za viza kutumia muda mrefu katika Terminal Two, mfano viza ya Ujerumani inakuwa ngumu kushughulikiwa na mashine hizo.

Pia alitaka mlolongo mrefu wa malipo katika benki ya NMB pale kiwanjani cha JNIA Terminal Two kutatuliwa haraka ili kuwapunguzia muda wasafiri.

Mkandarasi anataka kufanya vitu vya ziada na tayari wameshaelekezana naye na atavifanya, kwani viko ndani ya mkataba.

Amesema mikataba mipya katika eneo hilo la Terminal Three litakapokamilika, kipaumbele watapewa wafanyabiashara wazalendo, lakni wale wasafi wasiokuwa wababaishaji.

Naye  Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela amesema kuwa sehemu hiyo ya Termila Three itakapokamilika itahudumia Abiria milioni 6 kwa mwaka, ambao watakuwa wakihudumiwa kwa haraka na kwa nafasi na kuwepo sehemu bora ya kufanya biashara kuliko Terminal Two.

Huduma kwa abiria itakuwa bora zaidi kuliko kule kwa sababu eneo hilio ni la kisasa zaidi.

"Kutokana na huduma bora na ukubwa wa eneo tunatarajia kupata abiria wengi zaidi, "amesema.

Alisema kuwa jengo chakavu la Terminal Two litafanyiwa ukarabati ili kuwa la kisasa, ambapo mifumo mbalimbali itaboreshwa ili kuwahudumia abiria kwa haraka zaidi.

Amesema anaishukuru Serikali kwa kuisaidia TAA katika shughuli mbalimbali kama alivyoahidi Naibu Waziri.

"Kupitia Wizara, huduma mbalimbali zitaboreshwa kama alivyosema Naibu Waziri tupeleke bajeti yetu ili waweze kutusaidia, "amesema.


Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Johannes Munanka amesema kuwa kutakuwa na programu maalum ya kuutangaza uwanja huo kwa wananchi, ambapo aliwataka kuutembelea ili kuona shughuli zake na kujifunza mambo mbalimbali.




Ofisa Usalama wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Imani Mwakiyaragwe akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasilian) (kushoto) , Atashasta Nditiye  . Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Richard Mayongela.

No comments:

Post a Comment