Monday, 30 October 2017

Nyalandu atema ubunge na nyadhifa zote CCM

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (pichani), leo ametangaza rasmi kujiondoa katika Chama cha Mapinduzi na kuomba kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo au Chadema.

Kauli hiyo ameitoa leo, ambapo alisema anajivua nyadhifa zote alizonazo ndani ya Chama cha Mapinduzi, ukiwemo Ubunge, mbao ameutumkia kwa zaidi ya vipndi vinne.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Singida, chama hicho mkoa humo kimebainisha kufurahishwa na hatua hiyo na kudai kuwa alikuwa mzigo jimboni kwake.

Nyalandu baada ya kutangaza kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge wa Singida Kaskazini na kuihama CCM, alikiomba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumpokea.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida Martha Mlata, alisema pamoja na kwamba hajapata taarifa rasmi za kujiuzulu ubunge na kuhama chama kwa Nyalandu, amefurahi kama itakuwa ni kweli mbunge huyo ameachia nafasi ya ubunge.

“Mimi kama Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida nafurahi kama kweli ameondoka, kwa sababu kwa kweli alikuwa ni mzigo ndani ya chama. Nimeteseka sana kuliweka jimbo lake vizuri,” alisisitiza Mlata.

Alisema mbunge huyo alikuwa hatimizi majukumu yake ya kibunge ndani ya jimbo lake, hafanyi ziara zozote jimboni wala kuhudhuria vikao vya Bunge.

“Niseme ukweli tumefurahi na nina uhakika hata vijana wetu kule jimboni kwake wamefurahi. Afadhali maana ametusaidia kumpata mtu atakayelitendea haki jimbo lile,” alisema.

Awali, wakati akitangaza kuhama chama chake na kujiuzulu nafasi ya ubunge jijini Arusha leo, Nyalandu alisema ameamu kujiuzulu  nafasi zake zote ndani ya chama hicho ikiwemo ujumbe wa Halmashauri Kuu pamoja na nafasi zote za uongozi ndani ya Chama hicho.

Pia alisema tayari amemwandikia Spika wa Bunge Job Ndugai, barua ya kujiuzulu nafasi yake ya ubunge aliyoitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2000 hadi sasa.

Alisema amechukua  uamuzi huo  kutokana na kutoridhishwa kwake  na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu.

Aidha, alitaja sababu nyingine kuwa ni ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania wenzake na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya mihimili ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa kibunge wa kutunga sheria na kuisimamia serikali kutokuwa uhuru.


 “Najiuzulu nafasi zangu zote na naomba Chadema wanipokee kwa mikono miwili na pia natoa fursa kwa wananchi wachague mtu wanayemtaka  mara uchaguzi utakapotangazwa, lakini kwa sasa nakihama Chama cha Mapinduzi, “alisema.

No comments:

Post a Comment