Sunday, 29 October 2017
Wafanyakazi TAA kupatiwa mafunzo ya kazi
Na Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wataendelezwa kwa kupata mafunzo
mbalimbali, ili kuongeza weledi na tija kazini, imeelezwa.
Kauli hiyo ambayo
ni moja ya malengo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard
Mayongela jana alipoongea na wafanyakazi wa Kiwanja cha ndege cha Mwanza pamoja
na Kituo cha Zimamoto na Uokoaji, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi.
Bw. Mayongela
alisema wafanyakazi wakipata mafunzo
zaidi ya kazi zao wataisaidia serikari kufanikisha moja ya malengo yake makuu
ya kukuza uchumi, ambapo watakuwa na mbinu za kisasa zikiwemo za ukusanyaji wa
mapato kwa uaminifu na uadilifu, ambapo viwanja vya ndege ni moja ya vyanzo vya
mapato hayo.
Hata hivyo,
alisema atapitia majalada ya wafanyakazi
wote ili kubaini waliojiendeleza kwa mafunzo mbalimbali, lakini wanafanyakazi
zisizo za kada zao, hivyo ataangalia
uwezekano wa kuhamishiwa kwenye kada zao ili waweze kufanya kazi kwa weledi
zaidi.
“Wapo wafanyakazi
wa kada mbalimbali waliojiendeleza, lakini hadi sasa bado wapo kwenye kada
walizoajiriwa nazo na zipo tofauti na sasa, nitangalia uwezekano wa kupangiwa
kada zao ili waweze kuenda na kasi ya kazi zinazowahusu,” alisema Bw.Mayongela.
Pia malengo yake
mengine alisema atahakikisha anaboresha maslahi ya wafanyakazi wa ngazi ya
chini ili kunyanyua ari na tija kazini, ambapo kwa sasa wamekata tamaa kutokana
na maslahi duni yasiyolingana na kazi zao.
Lakini aliwaasa
wafanyakazi wenye mamlaka ya kuingia mikataba na wafanyabiashara, kubadilika na
kuhakikisha wanatumia vyema sheria zinazowaruhusu kuingia mkataba baina yao na
sio kukiuka, kwani inaweza kuwaletea matatizo, endapo itabainika kuwepo kwa
udanganyifu uliosababisha upotevu wa mapato ya serikali, kwa kuwa atahakikisha
TAA inajitosheleza kimapato na kujiendesha kwa baadhi ya mambo ya ndani bila kutegemea fedha kutoka
Serikali Kuu.
Alisema kwa sasa
TAA imekuwa ikinyooshewa kidole kwa kusemwa vibaya na wadau mbalimbali,
lakini kupitia umoja na mshikamano wa
wafanyakazi atahakikisha anarudisha taswira nzuri iliyokuwepo na kujenga
Mamlaka mpya yenye kuaminika.
Pia alizungumzia
uadilifu na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi, kuacha mara moja vitendo
vinavyoweza kuhujumu jitihada na vipaumbele kwa mwaka huu wa fedha 2017/18 hadi
kufikia 2020/21.
“Mimi ni mgeni
katika nafasi hii (ya Ukurugenzi), lakini ninachoomba tufanye kazi kwa bidii,
mvunje makundi na tukosoane kwa kujenga na sio kubomoa, na viongozi muache
kupendelea mtende haki kwa wafanyakazi wote, tukiwa na lengo la kuijenga TAA
yenye mwelekeo mpya,”alisema Bw. Mayongela.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment