Wednesday, 25 October 2017
TB Three kutumia mitambo ya Visa ya Elektroniki
Na Mwandishi Wetu
JENGO la tatu la
abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII)
linalotarajiwa kukamilika Desemba 2018, litafungwa mfumo wa huduma ya viza kwa
njia ya mtandao (e-visa), ambao utarahisha na kuharakisha upatikanaji wake.
Kaimu Mkuu wa
Kitengo cha Uhamiaji cha JNIA, Bw. Kaanankira Mbise amemwambia jana Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano),
Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye alipotembelea eneo la uombeaji viza kwa abiria
wa kimataifa wanaowasili, kuwa wanatarajia kutumia huduma hiyo ambayo ni rahisi
na haraka.
“Tayari mkakati
umeanza wa kuanzisha huduma hii ya e-visa hivyo tukifanikiwa utafungwa katika
jengo hili jipya, ambapo itasaidia kwa abiria kuipata huduma hiyo kwa haraka
kwani itatumia mtandao,” amesema Bw.
Mbise.
Hata hivyo, Bw.
Mbise amesema kwa sasa wameboresha huduma hiyo kwa wasafiri wanaowasili katika
jengo la pili la abiria (JNIA-TBII) , ambapo tayari wamepatiwa mashine nne za
kisasa zinazosaidia kupunguza msongamano wa abiria wenye kuhitaji huduma hiyo,
hususan kipindi cha mchana chenye ujio wa ndege nyingi za nje ya nchi.
“Hizi mashine
zimeharakisha upatikanaji wa huduma kwani tumeweza kuhudumia abiria wengi kwa
wakati mmoja, na msongamano umepungua kiasi tofauti na awali mashine zilikuwa
chache.” amesema Mbise.
Naye Mhe. Mhandisi
Nditiye amesema baada ya ziara yake amegundua mashine za viza ni za muda mrefu
na zinahudumia abiria mmoja kwa mrefu, na tayari ameuagiza uongozi wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuwasilisha kwa maandishi mapendekezo yao
ya namna ya kuharakisha huduma hiyo, ili serikali iyafanyie kazi kwa kusaidia
kuondoa kero hiyo.
“Nimegundua kuna
baadhi ya mashine za viza zimeongezwa lakini pia zilizopo zimechoka kwani ni za
muda mrefu na zinahudumia abiria mmoja kwa muda mrefu na hii inaharibu sifa ya
kiwanja chetu kwa wageni wanaokuja hapa nchini,” amesema Mhandisi Nditiye.
Hata hivyo,
amesema wanampango wa kuongeza madirisha ya benki yanayolipia viza hizo ili
kuharakisha huduma hiyo, ambapo sasa ni machache kulinganisha na idadi kubwa ya
abiria wanaowasili kwa ndege kubwa. Ndege hizo ni Emirates, Etihad, Oman Air,
Qatar, South Africa Air na Ethiopia, ambazo zimekuwa zikipishana kwa muda
mfupi.
Naye Kaimu
Mkurugenzi wa TAA, Richard Mayongela amesema tayari wanampango wa kuongeza
upana wa eneo hilo la wasafiri wanaowasili wa kimataifa, ambapo sasa kumekuwa
na msongamano kutokana na ufinyu wake.
“Hili jengo
linazaidi ya miaka 30 na ukiangalia abiria waliokuwa wamekadiriwa wakati ule
lilikuwa likikidhi mahitaji, lakini sasa abiria wameongezeka na eneo limekuwa
dogo, hivyo tayari tumeanza kwa kuondoa baadhi ya ofisi ili kuongeza upana
wake, ninaimani litapunguza msongamano uliopo sasa,” amesema Bw.
Mayongela.
Lakini pia Bw.
Mayongela amesema sasa wapo katika mazungumzo na Mamlaka ya Usafiri wa Anga
(TCAA), ili kuangalia namna bora ya kuzipangia muda ndege zinazopishana muda
mdogo kwa wakati wa mchana ili ziachiane muda mrefu, ambapo kutasaidia
kupunguza msongamano
Awali eneo hilo
linakumbwa na changamoto kubwa ya msongamano wa abiria wanaohitaji huduma ya
viza baada ya uchache mashine zinazosimamiwa na Idara ya Uhamiaji zilizokuwepo
na kufanya abiria wanaohitaji huduma hiyo kutumia muda mrefu kuipata.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment