Thursday, 19 October 2017
Naibu Waziri amtaka mkandarasi haraka
Na
Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa, amemtaka Mkandarasi wa
kampuni ya ujenzi ya China ya CHICO aliyepewa zabuni ya ujenzi wa Kiwanja cha
ndege cha Shinyanga kuanza ujenzi huo haraka.
Akizungumza mara
baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho katika eneo la Ibadakuli
leo, mkoani Shinyanga, Mhe. Kwandikwa, amesema kuwa haoni sababu ya mkandarasi
huyo kuchelewa kuleta vifaa vyake katika eneo la mradi hadi sasa wakati tayari
mkataba wa kuanza kazi hiyo umeshasainiwa.
"Mkandarasi
hana sababu ya kuchelewa kuanza kazi wakati fedha zipo na zimeshatengwa kwa
ajili ya mradi huu na mkataba umeshasainiwa,
sasa namwagiza kuleta vifaa vyake na kuanza kazi mara moja",
amesema Mhe. Kwandikwa.
Aidha, Mhe.
Kwandikwa amemtaka Meneja wa kiwanja hicho, Bw. Julius Msollow kuhakikisha
anakuwa bega kwa bega na kutoa ushirikiano kwa kumsimamia mkandarasi huyo, ili
kuhakikisha kiwanja hicho kinakamilika mapema na kwa viwango vinavyotakiwa.
"Naamini
tukimsimamia vizuri mkandarasi huyu tutapata kiwanja kizuri na imara hapa
Shinyanga na tutafungua fursa mbalimbali za kiuchumi katika mkoa huu",
amesisitiza Mhe. Kwandikwa.
Kwa upande wake,
Meneja wa kiwanja cha ndege cha Shinyanga, Bw. Msollow, amemhakikishia na
kuahidi kuwa atatoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo atakapowasili eneo la
mradi.
Bw. Msollow
amesema kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege,
jengo la abiria, maeneo ya maegesho ya ndege na mnara wa kuongozea ndege.
Amesema barabara
ya kutua na kupaa kwa ndege inarefushwa kwa urefu wa Kilometa mbili na itakuwa
kwa kiwango cha lami, ikigharimu zaidi ya shilingi Bilioni 49.
Wakati huohuo,
Naibu Waziri Kwandikwa, amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mwigumbi -
Maswa (KM 50.3), mkoani Simiyu na kumsisitiza mkandarasi anayejenga barabara
hiyo kuikamilisha kwa wakati na kwa viwango.
Amesisitiza kuwa
kukamilika kwa barabara hiyo ambayo ni kiungo kwa wananchi wa Maswa, Bariadi,
Lamadi na Mwanza, kutarahisisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo
katika maeneo hayo.
Naye, Meneja wa
Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Simiyu, Mhandisi Albert Kent, amesema
kuwa mradi upo katika hatua nzuri na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka
miwili kutoka sasa.
Naibu Waziri
Kwandikwa amefanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Shinyanga na Simiyu ambapo
amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment