Mafundi
wakiendelea na ukarabati katika jengo la abiria la Kiwanja cha Ndege wa Kimataifa
cha Kilimanjaro (KIA). Ukarabati huo unatarajiwa kukamilika Desemba 2017.
|
Thursday, 19 October 2017
Ukarabati KIA kukamilika Desemba 2017
KIWANJA
cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kinafanyiwa ukarabati mkubwa
unaohusisha miundombinu mbalimbali, ambapo unaotarajiwa kukamilika Desemba
2017.
Maeneo
yanayofanyiwa ukarabati ni pamoja na jengo la kupumzikia abiria, upanuzi wa
maegesho ya ndege na mifumo ya maji taka.
Akizungumza
baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati huo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Mhe. Elius Kwandikwa amesema ameridhika na hatua iliyofikia,
ikiwa ni zaidi ya asilimia 90.
"Nimeridhishwa
na ukarabati unaoendelea katika kiwanja hiki na nafikiri mmejionea wenyewe kazi
inaendelea vizuri, hivyo naamini kutokana na hali hii kazi itakamilika hivi
karibuni, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha,
Mhe Naibu Waziri amefafanua kuwa ukarabati huo ambao pia umehusisha maboresho
ya mfumo wa maji taka unalenga kuleta tija kwa mkoa huo na Taifa kwa ujumla
kutokana na kuwepo ongezeko la abiria, huduma za kijamii na kibiashara.
Amesisitiza
kuwa Serikali itaendelea kukarabati na kujenga viwanja vya ndege nchini ili
kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wananchi wake lengo likiwa ni
kuchochea fursa za kiuchumi ambazo zitasaidia kulipeleka Taifa katika uchumi wa
kati.
Naye Meneja
Miradi wa KIA, Mhandisi Mathew Ndossi,
amesema kuwa maegesho yatakapokamilika yatakuwa na uwezo wa kuegesha
jumla ya ndege kubwa 11 kwa wakati mmoja badala ya 6 zinazoegeshwa sasa.
Ameongeza
kuwa abiria wanatarajiwa kuongezeka kutoka 800,000 kwa mwaka hadi kufikia 1.2
milioni mara baada ya kukamilika kwa ukarabati huo.
Hivi
karibuni KIA imeandaa mbio za marathoni zitakazofanyika Novemba 19 kwa
kushirikisha raia mbalimbali wa nadani na nje ya nchi, ili kuvutia zaidi
watalii na watumiaji wa usafiri wa anga kwa ujumla.
Kia
pamoja na Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ni milango
ya kuingia nchini kwa usafiri wa anga kwa watalii wanaotoka nchi mbalimbali
duniani, kuja kutembelea mbuga za wanyama na
vivutio vinavyopatikana kwenye mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na
Zanzibar.
Wakati
huo huo, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua barabara ya Sakina - Tengeru (km 14.1)
na barabara ya mchepuko ya Arusha (Arusha Bypass km 42.4) ambapo amesema kuwa
kukamilika kwa barabara ya Sakina - Tengeru
ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na wageni wanaoingia
katika mkoa huo kwani kumepelekea
kupungua kwa ajali na msongamano
wa magari katika eneo hilo.
Ametoa
wito kwa wananchi kuzitunza barabara na
kutunza mazingira yanayozunguka barabara hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu
kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Naye,
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Arusha Mhandisi, Johny
Kalupale, amemhakikishia Naibu Waziri
huyo kufanya kazi kwa ubora na kwa weledi ili kutimiza malengo ya Serikali ya
kuwajengea wananchi miundombinu bora na ya kisasa.
Awamu ya
pili ya mradi huo sehemu ya barabara ya mchepuo ya Arusha (Arusha Bypass),
inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inatarajiwa kukamilika
mwakani na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 67.
Naibu
Waziri Kwandikwa amemaliza ziara ya kikazi katika mkoa wa Kilimanjaro na Arusha
ambapo amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment