Kikosi cha Yanga Africans. |
Na Mwandishi Wetu
KOCHA mkuu wa mabingwa wa soka Tanzania Bara,
Yanga, Hans van der Pluijm amesema kuwa, licha ya kupata ushindi mdogo wa 1-0
dhidi ya KMKM ya Zanzibar juzi kwenye Uwanja wa Taifa, lakini kikosi chake kipo
tayari kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame.
Pluijm alisema licha ya upungufu mdogo
uliojitokeza, ana matarajio makubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na
hata kulibakiza kwenye ardhi ya Tanzania kombe hilo ambalo linawaniwa na timu
13.
Michuano ya Kombe la Kagame inatarajia kuanza
jijini Dar es Salaam Julai 18 kwenye Uwanja wa Taifa.
Akizungumza juzi Pluijm alisema kikubwa kilichomvutia
katika mechi tatu za kirafiki walizocheza ni namna ambavyo timu hiyo ilivyokuwa
na uwiano baada ya kuziba nafasi za wachezaji ambao wameachana nao baada ya
msimu uliopita kumalizika.
“Naweza kusema hiki ndicho kikosi changu bora ukilinganisha
na kile kilichobeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kila mchezaji tuliyekuwa
naye msimu huu ana kitu cha ziada na wamekuwa na ushirikiano mzuri pamoja na
wale wageni,” alisema Pluijm.
Mholanzi huyo pia alisema amefurahishwa na
kiwango kilichooneshwa na mshambuliaji mpya raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma
ambaye ndiye aliyefunga bao hilo pekee katika mchezo na KMKM na kusema atakuwa na
mchango mkubwa kwenye kikosi chao na ni mmoja ya washambuliaji anayemtegemea
kufunga mabao mengi msimu huu.
No comments:
Post a Comment