Tuesday, 28 July 2015

Mapadri, mtawa wafa ajalini Kagera




Na Mwandishi Wetu
MAPADRI watatu na mtawa mmoja wa kanisa katoliki Jimbo la Rulenge Wilayani Ngara mkoani Kagera wamefariki dunia papo hapo huku watu 13 wakijeruhiwa, katika ajali ya barabarani wakiwahi Karagwe kwenye misa ya shukrani ya mwenzao aliyepata daraja hilo hivi karibuni.  

Katika ajali nyingine ya barabarani, watu saba wamekufa na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi na treni ya mizigo mkoani Tabora juzi.

Katika ajali hiyo, watu wanne walikufa katika eneo la tukio na wengine watatu kufia hospitalini baada ya kukimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ya Kitete.

Kwa mujibu wa moja wa mapadriwaliokuwa katika msafara huo, Erasto Nakule, ajali hiyo imetokea leo saa 2:00 asubuhi katika  barabara iendayo nchi jirani ya Uganda katika eneo la Bugorora  wilayani Missenyi mkoani Kagera.   

Alisema gari aina ya Land Cruser lenye namba ya usajili T.650 BYI la Jimbo Katoliki la Rulenge lililokuwa likiendeshwa na Padri Florian Tuombe ambaye amefia katika hospitali ya mkoa Kagera, liligongana uso kwa uso na basi la Kampuni ya Sabuni lenye namba za usajili T.166 AGU.  

Alisema basi la Sabuni lilikuwa likitokea wilayani Karagwe kwenda mkoani Mwanza, ambapo Land Cruser hilo lilikuwa likitokea Biharamulo kwenda Karagwe.

Padri Nakule aliwataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni pamoja na padri, Michael Mwelinde (70), Padri, Onesmo Buberwa (40), padre Florian Tuombe aliyekuwa dereva wa gari la mapadri na Sister  Magreth Kadebe (60).

Habari zaidi zilieleza kuwa mapadri hao walikuwa ni walimu wa seminari ya Rutabo wilayani Muleba na kwamba walikuwa wakienda kwenye misa ya shukrani ya padre Evisius Shumbusho  iliyouwa ikifanyika Karagwe.

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema chanzo cha ajali hiyo ni kutokana na dereva wa Land Cruser kuendesha bila kuchukua tahadhari, ambapo alitaka kupita basi la Sabuni na hivyo kugongana uso kwa uso. 

Kamanda Ollomi alisema katika ajali hiyo watu wanne wamefariki dunia na kwamba majina yao bado hayajajulikana akiwemo na mwanafunzi anayesomea upadri katika seminari ya Rutabo.

No comments:

Post a Comment