Na Mwandishi Wetu
Mwandishi wa habari na mtangazaji maarufu nchini, Abdallah Idrissa
Majura leo ameahidi kufanya mapinduzi ya michezo katika Jimbo la Kawe ambao
utakuwa ni mfano kwa maeneo mengine na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kurejesha fomu za
kuomba kugombea Ubunge Jimbo la Kawe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), alisema endapo atapendekezwa na kisha kuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo, ataanza na
michezo mitano ambayo ni soka, mpira wa kikapu, netiboli, wavu na mpira wa
mikono.
"Mungu akinijaalia nikatimiza ndoto yangu ya miaka mingi
nitaanza na michezo hii ambapo tutaunda timu moja yenye wachezaji mahiri katika
kila mchezo na zote zitajulikana kwa jina moja tu Kawe United," alisema
mtangazaji huyo ambaye pia ni mwanamichezo maarufu.
Alisema amekuwa akishangazwa kuona michezo kama mpira wa kikapu,
netiboli, wavu na mpira wa mikono haipigi hatua wakati haina gharama kubwa za
uendeshaji kulinganisha na soka, ambayo licha ya kuhitaji fedha nyingi pia kuna
ubabaishaji mkubwa ambapo viongozi wengi wanaoungoza mchezo nia yao ni kujinufaisha wenyewe binafsi.
Alisema kwa sasa hawezi kuweka wazi mikakati atakayotumia kuiinua michezo hiyo kwakuwa wakati wa kampeni haujawadia.Hata hivyo amesema ameamua kuanza na michache kwa sababu kipindi cha miaka mitano ni kidogo hivyo kama atabeba mzigo wa mambo mengi atashindwa kutimiza ahadi zake.
Mtangazaji huyo ambaye anamiliki kituo cha ABM FM RADIO cha mkoani
Dodoma amesema dhaimira yake ya kuinua michezo ilianza tangu mwaka 2010
alipoanzisha kituo hicho ambacho kinaongoza nchini kwakuwa na vipindi vingi vya
michezo kulinganisha na radio nyingine.ABM ina kipindi cha michezo kila baada
ya saa moja.
Kuhusiana na changamoto ya viwanja, mtangazaji huyo ambaye ameweka
rekodi ya kushinda tuzo za michezo za Baraza la Habari Tanzania (Ejat) kwa miaka
mitatu mfululizo huku mwandishi wake akishinda tuzo zilizopita, amesema anao
mkakati wa kuandaa uwanja mmoja ambao utatumia na timu zote za jimbo la Kawe
kwa ajili ya kufanyia mashindano.
"Kama nitapendekezwa na kisha kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Kawe
nimekusudia kuwashirikisha viongozi wenzangu jimboni tuuzungushie maduka uwanja
wa Tegeta Nyuki kisha tuuwekee majukwaa kama Azam Complex, naamini utakuwa ni
chanzo kizuri cha mapato ya jimbo na pia wanamichezo kuutumia.
Mgombea huyo amesema ameuchagua uwanja huo wa Tegeta Nyuki kwakuwa
ni mkubwa na pia ni rahisi kufikiwa na wanamichezo kutoka sehemu mbali mbali
kwani mabasi ya dalala dala yanaanzia hapo kwenda maeneo ya Kariakoo na Ubungo.
Majura ambaye pia amewahi kushinda tuzo ya Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo nchini (Taswa) 1997/98 zipo njia rahisi za kupata fedha za
kujenga maduka ya kuzunguka uwanja huo pia kutengeneza majukwaa na kuahidi
mbinu hizo kuziweka hadharani pindi kampeni zitakapoanza rasmi.
Mtangazaji huyo maarufu wa vipindi vya michezo ambaye amewahi
kufanyakazi radio Tanzania,radio one/itv na BBC licha ya kuwa na diploma ya
uandishi wa habari kutoka Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ), pia anayo
shahada ya kwanza ya Sayansi ya Jamii kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
No comments:
Post a Comment