WATANZANIA wameaswa kulinda amani na utulivu kuelekea
Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais mwezi Oktoba.
Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim
kwenye ufunguzi wa Semina ya siku tatu
ya Urithi wa Utamaduni wetu iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha kiislam (Muslim
University of Tanzania) kupitia taasisi
yake ya Urithi wa Utamaduni (Institute of Cultural Heritage).
“Cha msingi kuelekea uchaguzi mkuu, niwaombe watanzania
kulinda amani na utulivu kwenye nchi yetu ili kuendeleza sifa hii nzuri
inayotambulika kimataifa.
“Sasa tusiridhike na kujisahau tukaacha amani tuliyonayo
ikapotea, ni muhimu kulinda amani ya nchi yetu, tusichukulie yanayotokea katika
nchi nyingine ni ya uko uko tu, wote tuna wajibu wa kulinda amani ya nchi,”alisema
Dk Salim ambae pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Dk Salim alisema
kwamba demokrasia imekuwa kwa kiwango kikubwa na hiyo inafanya watu kuwa na
fikra tofauti na kusisitiza kwamba hakuna budi kukubaliana na fikra tofauti
kwani ni matokeo ya kukuwa na kupanuka kwa demokrasia nchini.
“Kuna vyama vingi vya siasa nchini, vikubwa na vidogo, yote
ni kutokana na kukua kwa demokrasia, uwingi wa vyama hivi unakuja na mawazo na
fikra tofauti tofauti na hivyo hatuna budi kukubaliana navyo kwani wote ni
watanzania,”alisema Dk Salim.
Alisema kwamba taifa linakabiliwa na changamoto kubwa ya
ukosefu wa maadili unayofanya watu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa
lengo la kwenda kula na sio kuwatumikia watanzania na kusema hali hiyo sio
vyema ikiachwa iendelee kwa mustakabali mzuri wa taifa.
No comments:
Post a Comment