Na Mwandishi Wetu
NYOTA wa kimataifa wa Simba waliokuwa na kikosi cha timu ya
taifa ya Uganda, The Cranes, beki Juuko Murshid na mshambuliaji, Emannuel Okwi
wanatarajiwa kutua jana jijini Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu
Tanzania Bara dhidi ya Azam FC utakaofanyika jesho Jumamosi kwenye Uwanja wa
Azam Complex.
Akizungmza Waandishi wa Habari kweye ukumbi wa mikutano wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya
Simba, Haji Manara amesema kwamba Juuko na Okwi walitarajia kutua jana na kujiunga
na wenzao kambini kwa ajili ya mchezo huo.
“Akina Okwi tunawatarajia kufika leo (jana) kutoka Uganda na watajiunga moja kwa moja na
wenzao kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya Azam,” amesema
Manara.
Ofisa huyo wa Simba amesema mchezo huo utakuwa mgumu kwa
sababu Azam ni timu nzuri na wao wamejipanga vizuri ingawa bado wana majeruhi
wawili tu, kipa Said Mohammed ‘Nduda’ na beki Shomari Kapombe.
Manara amesema kwamba Kapombe ataanza mazoezi Jumatatu wakati
Nduda ataondoka wikiendi hii kwenda India kwa ajili ya upasuaji wa goti.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga
amesema kwamba kikosi chao kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo huo na
watajitahidi kuvuna pointi tatu ili kuonyesha thamani ya kucheza nyumbani.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu, Simba ni timu nzuri na
tunatarajia mchezo utakuwa mgumu, lakini tunaamini pia ubora wa kikosi chetu na
maandalizi ni silaha yetu nzuri ya ushindi siku hiyo,”amesema Maganga.
Mapema katika Mkutano huo, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas
alisema kwamba mchezo huo utachezeshwa na refa Ludovick Charles wa Tabora,
atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Abdallah Mkomwa wa Pwani na
mezani atakuwepo Josephat Bulali na Kamisaa
atakuwa Ruvu Kiwanga, wote wa Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment