Wednesday, 13 September 2017

Mashindano ya taifa ya riadha kwa wanawake kufanyika Novemba ili kuchagua timu ya Olimpiki

Na Mwandishi Wetu

MASHINDANO ya riadha ya taifa ya wanawake yatafanyika jijini Dar es Salaam Novemba 24 na 25 kwa ajili ya kuchagua wachezaji watakaoingia kambini kwa maandalizi ya Michezo ya Olimpiki.

Timu hiyo hiyo itaingia kambini kwa ajili ya kushiriki mashindano mbalimbali ya kufuzu ili kufikia viwango vya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya 2020 itakayofanyika Tokyo, Japan.

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja (pichani) alisema jijini Dar es Salaam juzi kuwa, lengo la mashindano hayo ni kuongeza idadi ya wachezaji wakike katika Olimpiki hiyo ya Japan.

Alisema Ubalozi wa Japan kwa kushirikiana na BMT wameandaa program hiyo ili kuhakikisha Tanzania inapeleka wanariadha wengi wakike katika Michezo ya Olimpiki ya 2020.

Kiganja alisema kuwa baada ya  mashindano hayo ya taifa watatangaza wanariadha watakaoingia kambini ili kuwaandaa kwa mbio mbalimbali zitakazowawezesha kupata viwango vya kushiriki Olimpiki.

Aliiomba mikoa kuwaandaa wanariadha hao wakike kwa kuandaa mashindano ya mikoa ili kupata timu ya wachezaji sita watakaoshiriki mashindano hayo ya taifa jijini Dar es Salaam.

Alisema lengo lao ni kuhakikisha timu ya Tanzania inakuwa na wanariadha wengi wakike watakaoshiriki michezo hiyo inayofanyika kila baada ya miaka minne.

Wakati wa mashindano hayo wanariadha hao watagharamiwa malazi na chakula huku wakitakiwa kujigharamia nauli za kwenda na kurudi jijini Dar es Salaam.


Zaidi ya sh milioni 45 zinatarajia kutumika kwa ajili ya mashindano hayo ya kuchagua timu ya taifa pamoja na gharama zingine.

No comments:

Post a Comment