Thursday, 7 September 2017

Kibira achukua fomu kutetea kiti chake Chaneta

Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Annie Feith Kibira ni miongoni mwa wadau wa mchezo huo waliojitokeza kuchukua fomu kutaka kutetea au kuwania uongozi wa chama hicho.

Kibira na baadhi ya viongozi wenzake wanaoiongoza Chaneta, walifika katika ofisi za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kuchukua fomu kutaka kutetea nafasi zao katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Septemba 30 mjini Dodoma.

Ofisa Michezo wa BMT wa dawati la netiboli, Halima Bushiri amesema kuwa Kibira amechukua fomu kutaka kutetea kiti chake hicho katika uchaguzi ujao.

Bushiri aliwataja wengine waliochukua fomu jana kuwa ni pamoja na kaimu katibu mkuu wa Chanetam, Hilda Mwakatobe anayewania ukatibu msaidizi na ujumbe, Judith Ilunda anayeutaka ukatibu mkuu na ujumbe.

Wengine ni Julieth Mndeme (ujumbe), Mwajuma Kisengo, Asha Sapi, Kilongozi Mohamed.
Bushiri alisema mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Septemba 14 wakati tarehe ya usaili itapangwa na Kamati ya Uchaguzi itakayochaguliwa hivi karibuni.
Aliwataka wadau wa michezo wenye uwezo bila kujali jinsi zao kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu na kuzirejesha kwa wakati ili kuwania uongozi katika chama hicho.


Awali, uchaguzo huo ulipangwa kufanyika mjini Arusha lakini ulihamishiwa Dodoma baada ya kubaini kuwa Chama cha Netiboli Mkoa wa Arusha kilikuwa bado hakijafanya uchaguzi, hivyo kingekosa sifa za kuhudhuria mkutano huo.

No comments:

Post a Comment