Tuesday, 12 September 2017

Messi aing'arisha Barca, PSG, Chelsea, United zaua

ZURICH, Uswisi

NYOTA Lionel Messi alifunga mara mbili wakati Barcelona ikipata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Juventus katika moja ya mechi za ufunguzi za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, wakati vigogo vya soka vya Ufaransa Paris Saint-Germain, Manchester United na Chelsea nazo zikishinda kwa kishindo.

Baada ya kipindi kibaya cha majira ya joto, Barca ilikutana na washindi hao wa pili wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu uliopita, kitu ambacho Barcelona ilikuwa haikitaki cha kukutana na wakali hao wa Italia, lakini Messi alikuwa katika kiwango chake bora na kuipatia Catalans pointi zote tatu.

Mchezaji mpya Ousmane Dembele aliyeichezea kwa mara ya kwanza timu hiyo katika Ligi ya mabingwa kwenye Uwanja wa Camp Nou lakini alikuwa Messi ndiye aliyekuwa wa kwanza kufunga bao baada ya kugongeana vizuri na Luis Suarez.

Ulikuwa mchezo mzuri kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina ambao ulisaidia Ivan Rakitic aliyeifanya Barca kupata bao la pili katika dakika ya 56 na Messi aliongeza bao jingine na kuifanya timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 3-0 baada ya kufunga bao safi katika kipindi cha pili.

"Mara nyingi nilikuwa matata kwa kucheza dhidi ya Messi na sasa nina bahati kuwa na mchezaji huyo upande wangu, “alisema kocha wa Barcelona Ernesto Valverde.

Matokeo hayo yanaifanya Barcelona kulipa kisasi cha kufungwa na Juventus msimu uliopita baada ya Barca kufungwa katika robo fainali ya mashindano hayo na kuifanya kuongoza Kundi D pamoja na Sporting Lisbon, ambayo ilishinda 3-2 ugenini dhidi ya Olympiakos nchini Ugiriki.

Sporting, ambayo ilikuwa mbele kwa mabao matatu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, itakutana na Barcelona katika mchezo ujao utakaofanyika Ureno.

Wakati Barcelona ikizoea kucheza maisha bila ya Neymar, Mbrazil huyo amekuwa akifurahia maisha na PSG, ambapo alifunga bao la kuongoza wakati timu yake hiyo mpya ikishinda 5-0 dhidi ya Celtic katika mchezo wa Kundi B uliofanyika Glasgow.

Katika mchezo mwingine wa Kundi B, CSKA Moscow ilitoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mabingwa wa Ureno Benfica katika mchezo uliofanyika Lisbon, Ureno. CSKA itaikaribisha Man United baadae mwezi huu.

Klabu yazamani ya Mourinho, Chelsea ilipata ushindi mnono usiku huo, baada ya kuisasambua Qarabag 6-0 katika mchezo wa Kundi C uliofanyika kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

 

No comments:

Post a Comment