Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA wa Tanzania, Josephat Joseph, Ismail Juma na Gabrie Gerald
watalamba kitita cha Dola za Marekani 15,000 (sawa na Sh 33,540,000) endapo
watashinda mbio za kilometa 10 za Bolder Boulder zitakazofanyika Jumatatu Marekani.
Waandaaji wa mbio hizo wameandaa kiasi cha dola za Marekani 42,000
(sawa na Sh milioni 94) ikiwa ni zawadi kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa tano
kwa wanaume na wanawake.
Wanariadha wawili wa Tanzania, Joseph na Juma
waliondoka nchini juzi kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro
kwenda Colorado, Marekani ambako wataungana na Gerald kwa ajili ya mashindano
hayo.
Taarifa za mtandao zilisema kuwa dola 15,000 zinatolewa kwa timu
itakayoshinda ambayo itakuwa na wanariadha watatu huku zawadi binafsi kwa
mshindi wa kwanza ni dola 3,000.
Kwa mujibu wa waandaaji, mbio hizo ndizo hutoa
zawadi za fedha nyingi kuliko mbio zozote zisizo za marathoni Marekani, ambapo
hutoa kiasi cha dola 10,800 katika zawadi binafsi kwa ajili ya washindi 10 wa
kwanza.
Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania, Wilhelm Gidabuday alisema juzi kuwa
vijana hao baada ya mbio hizo wanatarajia kutembelea katika Chuo Kikuu cha Adam
State kilichopo Almos katika Jimbo la Colorado, Marekani.
No comments:
Post a Comment