Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania, RT, Wilhelm Gidabuday akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Tullo Chambo. |
Na Mwandishi Wetu
RIADHA Tanzania (RT) imewashukuru wadau waliofanikisha kufanyika kwa
mafanikio mashindano ya 12 ya riadha ya vijana wenye umri chini ya miaka 18
jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya vijana yaliyofanyika
kwenye Uwanja wa Taifa na Tanzania ilitwaa ushindi wa kwanza kwa upande wa
wanawake huku ikishika nafasi ya pili katika ushindi wa jumla.
Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday aliwashukuru wadau, kampuni na
watu mbalimbali waliofanikisha kufanyika mashindano hayo ya vijana.
Gidabuday alisema kuwa mashindano hayo yalifanikiwa na kufanyika kwake
kumewezesha wanariadha 17 wa Tanzania kufuzu kwa mashindano ya dunia
yatakayofanyika Nairobi, Kenya Julai 12 hadi 16.
Alisema kama wadau wangeshindwa kujitokeza kusaidia kufanyika kwa
mashindano hayo na RT ingeshindwa kuyaandaa, “basi wanariadha wetu wasingeweza
kufuzu kwa mashindano hayo ya Dunia.”
Alisema Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) limeipa Tanzania nafasi
mbili tu ya kushiriki mashindano hayo, ambao itawagharamia, huku RT ikisaka
fedha kwa ajili ya kuwagharamia wanariadha 15 waliobaki.
Aidha, Gidabuday alisema kuwa, RT pia itajitahidi kupeleka wanariadha
wengi katika mashindano ya dunia ya wakubwa yatakayofanyika London, Uingereza
Agosti.
Pia alisema kwa sasa wanasaka fedha kwa ajili ya kambi za timu hizo
mbili, ya vijana na ile ya wakubwa ili kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri
katika mashindano hayo yote.
Wadhamini wa mashindano hayo ni NMB, PPF, Vodacom, Serengeti Marathon na
Maji Uhai.
No comments:
Post a Comment