Na Waandishi Wetu
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Leo
ataongoza maelfu ya wananchi kuaga miili ya wanafunzi 33 na wafanyakazi watatu
wa shule ya Lucky Vicent ya Arusha waliokufa katika ajali ya gari katika
korongo la Mto Marera, Kata ya Rhotia wilayani Karatu mkoani Arusha.
Wanafunzi hao walikuwa wakienda Karatu kwa ajili ya mitihani ya kujipima
ya ujirani mwema kati ya shule yao na ile ya Tumaini ya Karatu.
Tangu baada ya taarifa za ajali za msiba huo kusambaa katika mitandao ya
kijamii, siku nzima ya juzi ikawa ya majonzi makubwa, ambayo yameendelea kwa
siku nyingine ya jana na zaidi leo wakati wa ibada maalumu kwenye Uwanja wa
Michezo wa Sheikh Amri Abeid Kaluta uliopo katikati ya Jiji la Arusha.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alitarajia kutua mjini Arusha jana jioni
na leo ataongoza wakazi hao wa Arusha pamoja na vitongoji vyake kuaga miili
hiyo.
Mbali ya Makamu wa Rais, viongozi wengine wa serikali watakaoshiriki
ibada hiyo ni Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Waziri wa
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu, Waziri wa
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
Tayari Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mstaafu,
Fredirick Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa wameshafika kwenye Uwanja
huo wa michezo kwa ajili ya hafla hiyo ya maombolezo.
Gambo atoa
ratiba
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aliwaambia wanahabari kuwa viongozi
hao wamethibitisha kushiriki ibada hiyo itakayoanza saa mbili asubuhi.
Gambo alisema miili yote ya wanafunzi waliokufa katika ajali hiyo
itakuwepo kwenye uwanja huo na kufanyiwa ibada kabla ya kuchukuliwa na ndugu,
jamaa kwa ajili ya kwenda katika maziko mahali watakapokuwa wamekuchagua.
Aliwataka Watanzania waliopo jijini Arusha na nje ya Arusha kuja kwa
wingi katika ibada hiyo yenye simanzi kubwa kwa Watanzania wote kote nchini.
Wanafunzi hao walipata ajali katika eneo la Rhotia na gari aina ya
Mitsubishi Rosa lenye namba za usajili T871 BYS lililokuwa likitoka jijini
Arusha kwenda katika Mji wa Karatu kupata ajali ya kutumbukia mtoni na
kusababisha vifo hivyo.
Wanafunzi hao waliondoka jijini Arusha saa mbili asubuhi kuwahi mtihani
huo wa majaribio wa kirafiki na wenzao wa Shule ya Msingi ya Tumaini Junior ya
Karatu.
Majina ya
waliokufa
Majina ya wanafunzi walikufa wametajwa kuwa ni Aisha Said, Anold Alex, Gladness Goodluck, Junior Mwashuy,
Praise Ronald, Witness Moses na Heavenlight Mcharo.
Wengine ni Eliapenda Eliudi, Rukia Halfan, Justine Alex, Rehema Msuya,
Irene Kishari, Prisca Charles, Ian Tarimo, Shedrak Bikhet, Sabrina Saidi,
Rachel Gidion, Irene Moses, Hagai Lucas.
Pia wamo Rehema Eliwadi, Rebeca Daudi, Dismas Kessy, Innocent Papian
(mwalimu), Oumuh Rashid, Gema Gerald, Grayson Masawe, Julius Bonge Mollel
(mwalimu), Joel Lucas, Naomi Hosea, Ruth Ndemno, Saada Ally, Neema Martin,
Witness Philemon na Musa Khamis.
Aidha, kwa mujibu wa mtu wa mtumishi wa chumba cha maiti Hospitali ya
Mkoa ya Mount Meru, ambaye hakupenda kutaja jina lake, baadhi ya miili ya
watoto hao imehamishiwa Hospitali ya Selian kwa sababu mochwari ya Mount Meru
ilikuwa imejaa, hivyo maiti zilizohamishiwa huko ni saba ambazo ni Neema
Martin, Oumuh Rashid, Gema Mchome, Irene Moses, Rebeka Daudi, Hagai Lucas na
Rachel Gidion.
Wazazi na walezi walikusanyika tangu asubuhi ya jana kwenye Hospitali ya
Mount Meru kwa ajili ya kuwaona watoto hao huku wakisoma majina yaliyobandikwa
ili kujua kama wapo hospitali hiyo au Hospitali ya Selian.
Wazazi wasimulia walivyopokea msiba
Katika hatua nyingine, badhi ya wazazi wameelezea jinsi walivyopokea
msiba kwa huzuni na wengine wakisema ni jambo la kushukuru kwa yote kwani
mapenzi ya Mungu yametimizwa.
Wakizungumza katika maeneo tofauti ya Kwamrombo katika eneo la Baa Mpya
na Mtaa wa Mlimani Kata ya Terrat, baadhi ya wazazi hao walioondokewa na watoto
wao, walisema inaumiza kwani baadhi ya watoto walikuwa wakikaa shuleni wakiwa
darasa la saba huku wengine wakitokea nyumbani kwenda ziara ya kimasomo Karatu.
Mzazi wa marehemu, Irene Moses (13) ambaye ni Mosses Kivuyo anayefanya
kazi Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga
ambaye sasa yupo masomoni Chuo cha Ufundi Arusha, alisema mtoto wake Irene
alikwenda Karatu na wenzake, lakini ghafla alisikia taarifa kuwa watoto hao
wamepata ajali.
Alisema hakujua kama mwanawe ni miongoni mwa waliokufa, lakini alijipa
moyo na kisha kuanza safari ya kutoka Arusha kwenda Rothia kwa ajili ya kuona
watoto hao akiwemo mwanawe Irene na alipokuwa njiani, alipigiwa simu na wauguzi
wakisema mtoto wake anataka kufanyiwa upasuaji, lakini wameamua kwanza wampigie
simu.
Ashuhudia mwanawe akikata roho
Alisema aliwajibu wauguzi hao kwamba yuko njiani anakwenda na
alipokaribia eneo la tukio hakumwona binti yake hivyo akaenda hospitali sababu
alipigiwa simu kwani mtoto wake ndiye alisema apigiwe simu akiwa majeruhi
“ndipo niliondoka kwenda kumuona Hospitali ya Karatu kumuona ndipo nilipofika
tu mtoto wangu namuona akifa.”
“Ukweli nimeumia kama mzazi. Huyu ni mtoto wangu wa kwanza kati ya watoto
watatu sasa huu msiba ni mzito sana kwetu wazazi tulioondokewa na watoto...
inauma jamani, lakini haya ni mapenzi ya Mungu nashukuru kwa hili. Lakini
nimeumia nafika tu hospitali mtoto anakufa jamani Irene wangu,” alieleza Moses.
No comments:
Post a Comment