Monday, 1 May 2017

Tottenham yazidisha presha kwa vinara Chelsea

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger (kushoto) na mwenzake wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino kabla ya kuanza kwa mchezo wa timu zao, ambapo Arsenal ilichapwa 2-0 juzi. 
LONDON, England
USHINDI wa Tottenham dhidi ya Arsenal una maana kuwa umeongeza shinikizo la kisaikolojia kwa Chelsea katika kilele cha msimamo wa Ligi Kuu ya England, anasema kocha Mauricio Pochettino.

Kocha huyo Muargentina alisema juzi kuwa, ushindi wa mabao 2-1 ni muhimu kwa mashabiki wetu, wakati Spurs ikithibitisha kuhitimisha miaka 22 ya kusubiri kumaliza juu ya wapinzani wao hao wakubwa.

Lakini kocha huyo aliongeza "kitu muhimu" ni kuendelea kubanana na vinara Chelsea, ambayo iliifunga Everton kwa mabao 3-0.

"Tuko katika mbio na tofauti imerejea kuwa pointi nne kama mwanzo,alisema Pochettino.

"Sasa tunatakiwa kuelekeza nguvu zetu katika kila mchezo. Tuna mchezo mwingine mkubwa dhidi ya West Ham Ijumaa, ikiwa ni mpambano mwingine mgumu.

"Hiyo itakuwa nafasi ya kuongeza shinikizo la kisaikolojia kwa Chelsea. Tutacheza kabla yao, na kama tukishinda itakuwa shinikizo tosha la kisaikolojia na tutaangalia nini kitatokea wakati Chelsea watakapocheza dhidi ya Middlesbrough Jumatatu kwenye Uwanja wa Stamford Bridge."

Ushindi wa Chelsea dhidi ya Everton katika mchezo uliopigwa mapema juzi Jumapili umekipandisha kikosi hicho cha kocha Antonio Conte pointi saba dhidi ya mpinzani wake mkubwa, lakini sasa tofauti imerejea katika pointi nne baada ya Spurs nayo kushinda.

Lakini bao la 21 la Dele Alli katika klabu hiyo msimu huu na lile la penalti la Harry Kane yaliiwezesha Spurs kupata ushindi wa tisa mfululizo katika ligi, ikiongeza kipindi chao bora tangu Oktoba 1960, wakati waliposhinda mechi 13 mfululizo.

Chelsea imekuwa ikishikilia uongozi wa ligi tangu Novemba 5, na walikuwa wakiongoza kwa pointi tisa Machi 19.
Tangu wakati huo, Chelsea ilifungwa mara mbili, wakipokea kichapo kutoka kwa Crystal Palace na baadae Manchester United.

"Naweza kuwaelewa mashabiki wetu kuwa watafurahia sana kama tutamaliza tukiwa juu ya Arsenal, lakini sijisikii sawa nao kwa sababu kwangu mimi ni suala la kujaribu kutwaa taji na sio kuwa juu ya Arsenal tu, aliongeza Pochettino.

"Ni muhimu sana sasa kujaribu na kushinda mataji kila msimu, hilo ndilo lengo letu kubwa.

"Ni ukweli kuwa itakuwa ngumu kutwaataji lakini tutaangalia nini kitatokea.

Mchezo wa Jumapili ndio lilikuwa pambano la mwisho kucheza kwenye Uwanja wa White Hart Lane katika hali ya sasa.

Tottenham itakuwa ikicheza mechi zake za nyumbani kwenye Uwanja wa Wembley katika msimu wa mwaka 2017-18 wakati ujenzi ukiendelea kwenye uwanja wao mpya.

Uwanja huo mpya wa klabu hiyo utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 61,000 waliokaa ambao unajengwa jirani na makazi yao ya sasa.


Mechi zilizobaki za Tottenham 2016-17:

Ijumaa, Mei 5     West Ham (Ugenini)

Jumapili, Mei 14  Man Utd (Nyumbani)

Alhamisi, Mei 8   Leicester (Ugenini)

Jumapili, Mei 21 Hull (Ugenini)


Mechi zilizobaki za Chelsea 2016-17


Jumatatu, Mei 8 Middlesbrough (Nyumbanbi)

Ijumaa, Mei 12:   West Brom (Ugenini)

Jumatatu, Mei 15  Watford (Nyumbani)

Jumapili, Mei 21  Sunderland (Nyumbani)

Jumamosi, Mei 27  Arsenal (Fainali FA Cup)

Kwa mara ya mwisho Tottenham ilimaliza juu ya Arsenal ilikuwa mwaka 1995, wakati walipomaliza wa saba na the Gunners walimaliza katika nafasi ya 12.


No comments:

Post a Comment