Saturday, 13 May 2017

Mwakyembe afungua mashindano ya riadha Kanda ya Tano ya Afrika kwa vijana wa U-17

Wanariadha wa Tanzania baada ya kutwaa medali ya dhahabu katika mbio za kupokezana vijiti za meta  4 X 100 kwenye Uwanja wa Taifa leo.

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrson Mwakyembe amezitaka kampuni mbalimbali kujitokeza kwa wingi kudhamini mchezo wa riadha.

Mwakyembe aliyasema hayo leo mchana wakati akifungua mashindano ya riadha ya Kanda ya Tano ya Afrika kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana, ambako jumla ya nchi saba zinashiriki.
Alisema kuwa makampuni zaidi yanatakiwa kujitokeza kudhamini mchezo huo, ambao miaka ya nyuma uliipatia sifa kubwa sana nchi kwa wanariadha wake kama akina Juma Ikangaa, Filbert Bayi, Suleimana Nyambui na wengin kufanya vizuri kimataifa.

Mashindano hayo yamedhaminiwa na NMB, Vodacom, PPF na Serengeti Marathon.


Waziri huyo pia alisema kuwa Riadha Tanzania (RT) kama wangeitaarifu mapema wizara, basi uwanja huo ungejaa wanafunzi kushuhudia wenzao wakitimua mbio pamoja na michezo mingine ya riadha.
Mwakyembe alishuhudia baadhi yam bio, ambapo washiriki walichuana vikali katika mbio tofauti tofauti kama zile za kupokezan vijiti za Meta 400 x 100 kwa wanaume, meta 3,000, 800 na zingine.
Katika mbio za meta 100 wanawake, Winfrida Makenji wa Tanzania aliibuka wa kwanza kwa kutumia sekunde 12.7, huku Naila wa Sudan ya Kusini alishika nafasi ya pili kwa kutumia sekunde 12.65 na Zanzibar ilimaliza ya tatu kupitia Kazija Hassan Simai aliyetumia sekunde 13.05.
Katika mbio za meta 800 wasichana, Tanzania ilishika nafasi ya pili kwa kutumia dakika 2:13:51 kupitia kwa Regina Mpigachai huku mshindi akiwa ni Mkenya aliyetumia dakika 02:12:43 na watatu ni Dorcus Boniface wa Tanzania aliyemaliza kwa dakika  02:13:71.
Tanzania ilitamba katika mbio za fainali ya kupokezana vijiti meta 100 x 400 wasichana pale waliposhika nafasi ya kwanza kwa kutumkia  sekunde 51;41 wakifuatiwa na Zanzibar waliotumia sekunde 53:31.
Mashindano hayo yanamalizika leo kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo bingwa wa jumla atajulikana huku nchi za Tanzania, Zanzibar, Eritrea, Sudan Kusini, Kenya na Somali zikishiriki baada ya Uganda, Ethiopia, Djibout na Rwanda zikishindwa kushiriki kwa sababu tofauti tofauti.



  







Wanariadha wa Tanzania wa washindi wa mbio za kupokezana vijiti kwa wasichana wakiwa na kocha wao Robert Kalhae mara baada ya kushinda mbio hizo leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment