Friday, 26 May 2017

Lukaku kukipiga Dar es Salaam akiwa na Everton

Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Everton ya England inatarajia kuzuru Tanzania kucheza mechi za kujiandaa na msimu mpya wa 2017/18, tovuti ya klabu hiyo imeandika.

Taarifa hiyo imeandika Everton watatembelea Tanzania na itakuwa timu ya kwanza ya Ligi Kuu ya England kucheza mechi katika nchi za Afrika Mashariki.

Ziara hiyo ambayo itakuwa sehemu ya sherehe zao za udhamini mpya wa Kampuni ya SportPesa, itaifikisha Everton kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000 kucheza mechi Alhamisi ya Julai 13.

Tanzania na Kenya zitakutanisha timu nane, nne kutoka kila upande katika michuano ya SportPesa, kuwania nafasi ya kucheza Romelu Lukaku.

Mapema mwezi huu, Everton ilitangaza udhamini mnono wa rekodi na SportPesa wa miaka mitano na baada ya hapo kampuni hiyo ikaingia Afrika Mashariki kuingia mkataba na klabu kadhaa kubwa, zikiwemo Simba na Yanga.

Michuano ya SportPesa Super Cup inatarajiwa kuanza Juni 5 hadi 11 Dar es Salaam, ikishirikisha timu za Simba, Yanga, Singida United na Jang'ombe Boys za Tanzania, Gor Mahia, AFC Leopards, Nakuru All Stars na Tusker FC za Kenya.

Bingwa wa michuano hiyo itakayofanyika Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam ndiye atamenyana na Everton na pia ataondoka na kitita cha sh. milioni 60.


Everton imemaliza ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu ya England ikijikusanyia jumla ya pointi 61 huku Chelsea ikimaliza ya kwanza kwa kuwa na pointi 93 katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 20.

No comments:

Post a Comment