Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Tanzania Prisons leo ilimeichapa Shule ya Sekondari ya Makongo
wanawake kwa seti 3-0 katika mchezo wa mashindano ya Muungano ya mpira wa wavu
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wa Tanzania Prisons (kulia) wakichuana na wale wa Makocha Sekondari wakati wa mchezo wa mpira wa wavu wa Muungano leo kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Makongo imekutana na kipigo hicho ikiwa ni siku moja tu baada ya kuifunga
Jeshi Stars ambaye ni bingwa mtetezi kwa seti 3-1.
Katika mchezo huo, Tanzania Prisons ilishinda 25-20 katika seti ya kwanza,kabla
ya kuibuka na 25-23 katika seti ya pili huku katika seti ya mwisho ikitamba kwa
pointi 25-17.
Kwa upande wa wanaume, Kinyerezi iliifunga Mjimwema kwa seti 3-0, ambapo washindi
walifanya kweli kwa ushindi wa 28-26, 25-22 na 25-20.
Akizungumza kando ya mashindano hayo, Katibu Msaidizi wa Chama cha mchezo
wa Wavu Tanzania, (TAVA) Alfred Selengia alisema mashindano hayo yana ushindani
tofauti na mwaka jana.
“Mashindano yanaendelea vizuri na ushindani ni mkubwa tofauti na mwaka
jana. Bingwa atapata kombe na medali pamoja na mshindi wa pili,” alisema
Selengia.
Pia Selengia alisema bingwa ndiye atawakilisha nchi kwenye mashindano ya
Afrika yatakayofanyika mwakani kwa timu za wanawake na wanaume.
Timu zinazoshiriki ni bingwa mtetezi Jeshi Stars, Chui, Polisi Zanzibar,
Moro Stars, Makongo Sekondari, Tanzania Prisons, Saut Mwanza, Mafunzo ya
Zanzibar, Dodoma, Mjimwema, Victory Sports na Kinyerezi.
No comments:
Post a Comment