Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemfungia Mkuu
wa Idara ya Mawasiliano wa Simba, Haji Manara (Pichani), kujihusisha na masuala ya soka
kwa mwaka mmoja na kupigwa faini ya Sh. Milioni 9.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Jerome Msemwa amesema jijini Dar es Salaam leo
kuwa, hatua hiyo imefikiwa baada ya Manara kukutwa na makosa matatu dhidi ya
TFF waliomlalamikia.
Msemwa ameyataja makosa hayo kuwa ni kuituhumu na kuidhalilisha TFF,
kueneza chuki za ukabila na la tatu kuingilia utendaji wa shirikisho hilo.
Kwa makosa hayo yote, anakumbana na adhabu ya kuwa nje ya masuala ya soka
kwa mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh. Milioni 9 kabla ya kumaliza adhabu yake.
Kosa la kwanza amehukumiwa kwa mujibu wa kanuni ya 41 kifungu cha tisa, ambalo
alitakiwa alipe faini ya Sh. Milioni 1, la pili amehukumiwa kwa kanuni ya 53
kifungu cha kwanza na cha pili na anafungiwa miezi mitatu na faini ya Sh.
Milioni 3 na kosa la tatu amehukumiwa kwa kanuni ya kwanza na ya pili inayohusu
maadili, ambayo alitakiwa afungiwe miaka saba na faini ya Sh. Milioni 5.
Lakini kutokana na kuwa hilo ni kosa lake la kwanza Kamati imetumia
mamlaka yake kwa kumpunguzia adhabu hadi miezi 12 na faini ya Sh. Milioni 5 –
na adhabu hizo zimeunganishwa, hivyo atatumikia kifungo cha mwaka mmoja na
kulipa faini ya Sh. Milioni 9.
Hata hivyo, Msemwa alisema Manara hakutokea kwenye kikao cha kutoa
utetezi wake dhidi ya tuhuma hizo, ingawa taarifa ya kuitwa alifikishiwa yeye
na klabu yake pia.
Katikati ya wiki, Manara aliituhumu TFF kufanya njama za waziwazi ili
kuwabeba wapinzani wao, Yanga katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Manara pia aliwatuhumu viongozi wakuu wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu
wake, Selestine Mwesigwa ni wahaya na viongozi wa zamani wa Yanga, ambao
wanataka kuipendelea Kagera Sugar na timu hiyo yao hiyo ya zamani.
Hasira za Manara zilikuja baada ya TFF kulipeleka Kamati ya Katiba Sheria
na Hadhi za Wachezaji suala la Simba kupewa ushindi wa zamani na Kamati ya
Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72.
Kamati ya Saa 72 iliipa Simba pointi tatu na mabao matatu baada ya
kujiridhisha beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi aliichezea timu hiyo dhidi ya
Simba Aprili 2 akiwa na kadi tatu za njano, ikiwa ni kinyume cha kanuni.
Lakini siku mbili baadaye, Kagera Sugar wakapinga maamuzi hayo na kuomba
suala hilo lisikilizwe upya kwa kuwa mchezaji wao hakuwa na kadi tatu za njano
siku wanaifunga Simba 2-0 mjini Bukoba.
No comments:
Post a Comment