Na Mwandishi Wetu, Mwanza
SIMBA ya Dar es Salaam imekamilisha mechi zake za Kanda ya Ziwa kwa kuondoka na pointi saba baada ya jana kushindwa kuifunga Toto Africans katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.
Pointi hizo saba ilizopata Simba ni baada ya kupewa zile tatu za mezani walizopewa na Kamati ya Saa 72 baada ya Wekundu hao wa Msimbazi kukata rufaa kupinga Kagera Sugar kumchezesha kumchezesha Mohamed Fakhi aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Kwa matokeo ya mchezo dhidi ya Toto Africans, Simba wana pointi 62 huku ikishinda 3-2 katika mchezo wake wa kwanza Mwanza dhidi ya Mabao FC kwenye uwanja huo huo.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu hizo zilikuwa
suluhu licha ya kushambuliana kwa zamu kila moja ikisaka bao la kuongoza.
Simba ndio walikuwa wa kwanza kulifikia lango la Toto
Africans katika dakika ya pili, lakini Shiza Kichuya alishindwa kufunga,
alipaisha juu ya goli.
Dakika ya 37, Hamimu Abdul alipiga mpira katika lango la
Simba, lakini James Agyei akaicheza.
Kocha wa Simba, Joseph Omog alifanya mabadiliko kadhaa akiwatoa kiungo Mohammed Ibrahim na mshambuliaji Laudit Mavugo na kuwaingiza
Mwinyi Kazimoto na mshambuliaji Ibrahim Hajib.
Pamoja na mabadiliko hayo, mchezo uliendelea kuwa mgumu na
Omog akaamua kumtoa na winga Shiza Kichuya na kumuingiza mshambuliaji Juma
Luizio, wakati kocha wa Toto, Furgence Novatus alimtoa Jamal Mtengeta na
kumuingiza Hamad Nathaniel Mbumba.
Kosa kosa ziliendelea huku Simba wakilishambulia zaidi lango
la wapinzani wao, lakini walishindwa kupata bao na kulazimishwa suluhu.
Yanga ambayo haikushuka dimbani katika Ligi Kuu, wenyewe walicheza Algeria katika mchezo wa mchujo wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.
No comments:
Post a Comment