Friday, 14 April 2017

Ndondi wajichuja Michezo ya Jumuiya ya Madola Gold Coast, Australia 2018 kutokana na ukata

Kocha wa timu ya taifa, Mzonge Hassan akifuatilia  mazoezi ya mabondia wa timu hiyo kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Ngumi Tanzania (BFT) huenda likashindwa kupeleka mabondia katika Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Gold Coast mwakani kutokana na ukata, imeelezwa.

Akizungumza jana Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alisema kuwa wahawa uhakika wa kupeleka mabondia katika mashindano ya ndondi ya Afrika yatakayofanyika Brazzaville, Congo kuanzia Mei 27 hadi Juni 4.

Alisema kuwa wanakabiliwa na ukata, hivyo hawatapeleka mabondia katika mashindano hayo na hivyo kushindwa kufuzukwa mashindano ya dunia yatakayofanyika Hamburg, Ujerumani Agosti 25 hadi Septemba 3 mwaka huu.

Endapo watashindwa kufuzu kushiriki mashindano ya dunia, moja kwa moja mabondia wa Tanzania hawatakuwa na vigezo vya kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola pamoja na ile ya Olimpiki Japan 2020.

Mashaga alisema wamekata tamaa ya kusaka fedha, kwani kila wanakopiga hodi wanaambiwa kuwa hakuna fedha licha ya kupeleka maombi mapema.

Alipoulizwa kama anajua kuwa kushindwa kupeleka timu katika mashindano ya Afrika pamoja ya yale ya dunia kama kutawafanya kushindwa kupeleka timu katika Jumuiya ya Madola na Olimpiki, Mashaga alisema analijua hilo vizuri.

Juzi Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema kuwa ngumi hawana viwango vya kushiriki Jumuiya ya Madola, lakini lazima kwanza washiriki mashindano ya Dunia.
Alisema mchezaji hataruhusiwa kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola kama hajashiriki mashindano ya dunia ya mchezo wake.


Timu ya ndondi ilishindwa kushiriki michezo iliyopita ya Olimpiki iliyofanyika Rio de Janeiro, Brazil mwaka jana baada ya mabondia wake kutoshiriki mashindano ya dunia.

No comments:

Post a Comment