Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RIADHA Tanzania (RT) imezisimamisha mbio za Serengeti kwa muda
usiojulikana baada ya kuwepo ubabaishaji mkubwa wakati wa kuendesha mbio hizo
mwaka huu imeelezwa.
Kaimu katibu Mkuu wa RT, Ombeni Zavalla alisema jana kuwa, hatua
hiyo ilifikiwa baada ya kikao kilichofanyika katikati ya wiki hii kati ya Baraza la Michezo
la Taifa (BMT), RT na waandaaji wa mbio hizo kujadili mapungufu yaliyojitokeza.
Zavalla alisema kuwa, wamezisimamisha mbio hizo baada ya kubaini
mapungufu kibao yalijitokeza ikiwemo ubabaishaji katika zawadi, usimamizi na
utawala, ambavyo navyo havikuwa sawa sawa.
Akifafanua mapungufu hayo, Zavalla alisema kwa upande wa zawadi
waandaaji hao waliahidi kutoa sh.. milioni 1.5 kwa washindi wa kwanza na pili
kwa wanawake na wanaume wakati washindi wa pili kila mmoa alitakiwa kupewa
sh.milioni 1 na watatu sh. 500,000.
Lakini waandaaji hao walishindwa kutimiza ahadi hiyo kwa upande wa
zawadi, ambapo washindi wote walipewa fedha pungufu tofauti na walivyoahidiwa.
Alisema pia waandaaji hao waliendesha mbio hizo bila ya
kushirikiana na Chama cha Riadha cha Mkoa wa Simiyu, wanariadha walinusurika
kugongwa na magari baada ya kutokuwepo kwa watu wa usalama na hakukuwa na
wasimamizi wa kutosha na wenye uelewa wa mchezo huo.
Matatizo mengine yaliyoikeza ni pamoja na waandaaji wa mbio hizo
kutosajiliwa na kuwashirikisha wanariadha kutoka nje ya nchi kama Kenya bila
kuwaombea vibali RT.
Alisema ni kosa kubwa kwa waandaaji wa mbio kushirikisha
wanariadha wa nje bila ya kuwaombea vibali kwa RT.
Aidha, BMT imeiagiza RT kukutana na waandaaji wote wa mbio hapa
nchini na kuwapa mafunzo kuhusu taratibu zote za uandaaji wa mbio hizo ili
kuepuka migogoro katika mbio wanazoandaa.
No comments:
Post a Comment