Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Annie Kibira anaendelea
kupatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kupooza.
Kibira alianguka ghafla baada ya kupatwa na shinikizo la damu na
kuanguka wakati akisimamia mashindano ya netiboli ya Muungano kisiwani Zanzibar
na baadae kulazwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja kisiwani humo kabla ya
kuhamishiwa Muhimbili.
Mashindano ya Muungano ya netiboli yalimalizika wiki iliyopita
kwenye Uwana wa Gymkhana huku mabingwa wa Tanzania Bara Uhamiaji wakiibuka
mashujaa baada ya kulitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza.
Mtoto wa Kibira, Kelvin amesema kuwa mama yake kesho Jumanne
anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya MR1 katika hospitali hiyo kwa ajili ya
matibabu zaidi.
Alisema kuwa Kibira amelazwa Mwaisela word namba 7 chumba namba
311, ambako anaendelea na matibabu baada ya kupooza upande wa kulia kuanzia
mguuni hadi usoni.
Alisema kuwa kutokana na kuongozana kwa Siku Kuu za Maulidi,
Krismas na wikiendi, ndiko kulikosababisha mama yake kuchelewa kufanyiwa baadhi
ya vipimo.
Alisema kuwa leo Jumatatu mama alitarajia kuanza kufanyiwa mazoezi
ikiwa ni sehemu ya matibabu yake.
Akizungumzia hali ya mama yake, Kelvin alisema kuwa anaendelea
vizuri tofauti na alivyokuwa awali.
Kibira kabla ya mashindano hayo ya netiboli ya Muungano
alihudhuria Mkutano Mkuu wa kawaida wa mwaka wa Kamati ya Olimpiki Tanzania
(TOC) mjini Zanzibar, kabla ya kufanyika mashindano hayo ya Muungano, huku akiwa
mwenye afya tele.
No comments:
Post a Comment