Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) , Annie Kibira (kulia), wakati wa Mkutano Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ulifanyika Desemba 12 mwaka huu Zanzibar. |
Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Annie Kibira
aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar baada ya
kupooza ghafla, amehamishiwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu
zaidi, imeelezwa.
Kibira alianguka ghafla wakati akisimamia mashindano ya netiboli
ya Muungano yaliyokuwa yakifanyika kwenye Uwanja wa Gymkhana wiki iliyopita
baada ya presha kumpanda.
Mtoto wa Kibira aliyejitambulisha kwa jina la Kelvin amesema leo
asubuhi kuwa, mama yake jana alihamishiwa katika hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, ambako anatarajiwa kufanyiwa vipimo zaidi vya matibabu.
Alisema kuwa mama yake hospitalini hapo anasubiri kipimo cha MR1
kwa ajili ya uchunguzi zaidi, lakini anaendelea vizuri hospitalini hapo.
Mwanzoni mwa wiki Kibira akiwa amelazwa katika hospitali ya Mnazi
Mmoja alizungumza na mwandishi wetu na kusema kuwa alianguka uwanjani baada ya
presha kupanda, lakini alikuwa anaendelea vizuri.
Kibira alisema kuwa alipooza upande wa kulia kuanzia mguuni hadi
kichwani, lakini alikuwa akiendelea vizuri.
Kibira kabla ya mashindano hayo ya netiboli ya Muungano alihudhuria mkutano Mkuu wa kawaida wa mwaka wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), kabla ya kufanyika mashindano hayo ya Muungano akionekana mwenye afya tele, ambapo aliwapongeza TOC kwa maandalizi mazuri ya mkutano wao.
Kibira alisema kuwa, TOC ni mfano wa kuigwa kwa vyama na mashirikisho menggine ya michezo kwa kuandaa vizuri mikutano yao na kila mwaka kuendesha mkutano huo bila ya kukosa tofauti na vyama vingine.
Mungu amponye
haraka Kibira ili aendelee na shughuli za ujenzi wa taifa pamoja na mchezo wa
netiboli.
No comments:
Post a Comment