Wednesday, 16 December 2015

Mkuu wa Wilaya ya Karatu ndiye mgeni rasmi tamasha la michezo la mwaka huu la Karatu


Baadhi ya wanariadha nyota wa kike wakichuana katika mbio za kilometa tano za Karatu mwaka jana

Na Mwandishi Wetu
MKUU wa wilaya ya Karatu, Omary Kwaanq anataraia kuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa tamasha la michezo la Karatu Jumamosi Desemba 19 kwenye Uwanja wa Mazingira Bora, imeelezwa.

Mratibu wa tamasha hilo, ambalo hufanyika kila mwaka mjini Karatu, Meta Petro alisema kuwa, mkuu huyo wa wilaya ndiye atakayetoa zawadi kwa washindi wa michezo mbalimbali katika tamasha hilo.

Baadhi ya waratibu wa mbio hizo wakijadili mambo wakati wa mbio za mwaka jana.
Alisema kuwa mbali na riadha, ambayo itashindaniwa katika mbio za kilometa 10, tano na 2.5, pia kutakuwa na michezo ya mpira wa wavu, soka, mbio za baiskeli na burudani za kwaya na ngoma.

Akizungumzia riadha, Petro ambaye aliwahi kuwa mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania katika miaka ya nyuma alisema kuwa, wanariadha kibao nyota wamethibitisha kushiriki tamasha hilo katika mbio za kilometa 10 na tano, kwa wanaume na wanawake.
Wanariadha wa mbio za kilometa 10 za tamasha la Karatu wakijiandaa kuanza mbio za mwaka jana.
Aliwataja baadhi ya nyota waliothibitisha kushiriki mbio hizo kuwa ni pamoja na Fabian Nelson, bingwa wa mwaka huu wa Ngorongoro Marathoni Joseph Teophilo, bingwa wa Kilimanjaro Marathoni kwa wanawake, Abiola William na Bazil John.

Alisema kuwa mchezo wa soka ulianza leo Jumatano hatua ya wilaya, ambapo mshindi wa leo atacheza Ijumaa na mshindi wa kesho katika hatua ya fainali, ambapo mshindi ndiye atakuwa bingwa wa mwaka huu katika soka.
Mshindi wa mbio za kilometa tano kwa wanawake, Failuna Abdi akipewa zawadi na rais wazamani wa Riadha Tanzania, Francis John. anayeshuhudia ni mratibu wa mbio hizo, Meta Petro.
 Mbali na riadha na soka, mchezo wa mbio za baiskeli ambao huwa na msisimko wa aina yake,wenyewe utashindanisha washiriki katika umbali wa kilometa 60 kwa upande wa wanawake na wanaume.
Muandaaji wa tamasha la michezo la Karatu, Filbert Bayi (katikati), akiwa na washindi baada ya kukabidhiwa zawadi zao katika tamasha la mwaka jana mjini Karatu.

No comments:

Post a Comment