Na Mwandishi Wetu
MAPADRI watatu na mtawa mmoja wa kanisa
katoliki Jimbo la Rulenge Wilayani Ngara mkoani Kagera wamefariki dunia papo
hapo huku watu 13 wakijeruhiwa, katika ajali ya barabarani wakiwahi Karagwe
kwenye misa ya shukrani ya mwenzao aliyepata daraja hilo hivi karibuni.
Katika ajali nyingine ya barabarani, watu
saba wamekufa na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi na treni
ya mizigo mkoani Tabora juzi.
Katika ajali hiyo, watu wanne walikufa katika
eneo la tukio na wengine watatu kufia hospitalini baada ya kukimbizwa katika hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ya Kitete.
Kwa mujibu wa moja wa mapadriwaliokuwa katika
msafara huo, Erasto Nakule, ajali hiyo imetokea leo saa 2:00 asubuhi katika barabara iendayo nchi jirani ya Uganda katika
eneo la Bugorora wilayani Missenyi
mkoani Kagera.
Alisema gari aina ya Land Cruser lenye namba
ya usajili T.650 BYI la Jimbo Katoliki la Rulenge lililokuwa likiendeshwa na
Padri Florian Tuombe ambaye amefia katika hospitali ya mkoa Kagera, liligongana
uso kwa uso na basi la Kampuni ya Sabuni lenye namba za usajili T.166 AGU.
Alisema basi la Sabuni lilikuwa likitokea wilayani
Karagwe kwenda mkoani Mwanza, ambapo Land Cruser hilo lilikuwa likitokea Biharamulo
kwenda Karagwe.
Padri Nakule aliwataja waliofariki dunia katika
ajali hiyo kuwa ni pamoja na padri, Michael Mwelinde (70), Padri, Onesmo
Buberwa (40), padre Florian Tuombe aliyekuwa dereva wa gari la mapadri na Sister Magreth Kadebe (60).
Habari zaidi zilieleza kuwa mapadri hao
walikuwa ni walimu wa seminari ya Rutabo wilayani Muleba na kwamba walikuwa
wakienda kwenye misa ya shukrani ya padre Evisius Shumbusho iliyouwa ikifanyika Karagwe.
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera,
Augustine Ollomi alisema chanzo cha ajali hiyo ni kutokana na dereva wa Land Cruser
kuendesha bila kuchukua tahadhari, ambapo alitaka kupita basi la Sabuni na
hivyo kugongana uso kwa uso.
Kamanda Ollomi alisema katika ajali hiyo watu
wanne wamefariki dunia na kwamba majina yao bado hayajajulikana akiwemo na
mwanafunzi anayesomea upadri katika seminari ya Rutabo.