WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape
Nnauye atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha Tamasha la Michezo la Karatu kitakachofanyika
Jumamosi Desemba 17, imeelezwa.
Mratibu wa tamasha hilo, ambaye ia ni mwanariadha
wazamani na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Riadha Tanzania (RT), Meta Petro alisema
mjini hapa juzi kuwa, Waziri Nape ndiye atakuwa mgeni rasmi katika hitimisho la
tamasha hilo, ambalo hufanyika kila mwaka.
Mbali na mbio za kilometa 10 kwa wanawake na wanaume,
tamasha hilo pia limekuwa likishirikisha michezo ya mbio za baiskeli za
kilometa 60, mbio za watoto za kilometa 2.5 na michezo ya mpira wa wavu na
soka, ngoma za utamaduni, sarakasi pamoja na kwaya.
Kwa mujibu wa Petro, mchezo wa mpira wa wavu na soka,
fainali zake zitafanyika Ijumaa Desemba 16, lakini washindi watakabidhiwa
zawadi zao pamoja na wenzao wa riadha na baiskeli Jumamosi Desemba 17 siku ya
kilele cha tamasha hilo, ambalo hudhaminiwa na Olympic Solidarity kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na FBF.
Msisimko mkubwa unatarajiwa kuibuka katika mbio za
kilometa 10 kwa wanawake na wanaume pamoja na zile za baiskeli, ambazo
washiriki wake wengi wanatoka mjini Arusha na maeneo mengine ya Karatu, Mto wa
Mbu, Manyara na kwingineko.
Mechi za soka na mpira wa wavu ambazo huanzia ngazi
ya chini na kushirikisha timu kibao, kabla
ya kucheza fainali na kupata washindi wa michezo hiyo, ambao hukabidhiwa zawadi
nono kutoka kwa waandaaji,
Baadhi ya zawadi zinazotolewa na Taasisi ya Filbert
Bayi Foundation (FBF), ambao ndio waandaaji ni pamoja na fedha taslimu, mipira,
nyavu za magoli ya mchezo wa soka, jezi, glovu na vifaa vingine.
Pia kwa upande wa mchezo wa mpira wa wavu, vifaa
vinavyotolewa kwa washindi mbali na fedha taslimu ni pamoja na mipira, wavu za
kuchezea na vifaa vingine vya mchezo huo, ambyo mjini Karatu huchezwa zaidi na
timu za madhehebu ya kidini.
Petro alitaka wanariadha watakaoshiriki mbio hizo
wajitahidi kujisajili mapema ili kujua idadi kamili ya watakaoshiriki badala ya
kusubiri siku ya mwisho ndio kujitokeza, kwani ina wapa wakati mgumu waandaaji kupanga
taratibu mbalimbali.
Kwa ujumla zawadi katika michezo mbalimbali ya Tamasha la Karatu ni za kuvutia na zimeanufaisha wanamichezo binafsi na timu kwa kupata fedha taslimu na vifaa vya michezo, ambavyo vinasaidia kuongeza ari ya kushiriki katika michezo na kuinua vipaji.
No comments:
Post a Comment