Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Multchoice-Tanzania mapema leo imekabidhi
msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh. Milioni 5 kwa Kituo cha Watoto
Yatima cha Al-Madina kilichopo Tandale kwa Tumbo jijini Dar es Salaam kwa ajili
ya Siku Kuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Msaada huo uliohusisha sare za shule, unga wa ngano,
unga wa mahindi, biskuti, juice za aina mbalimbali, soda, mafuta ya kupikia,
mchele na nguo zingine ulitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice-Tanzania,
Maharage Chande kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, ambao baadhi yao aliambatana
nao hadi Uswazi.
Vingine walivyokabidhi leo ni pamoja na vyombo vipya
kabisa vya kulia chakula, fedha taslimu za kusaidia kulipia gharama zao za
pango wanapoishi watoto hao na vitu vingine.
Akizungumza kabla ya kumkabidhi msaada huo, Chande
alisema kuwa kampuni yao kwa miaka mingi imekuwa na mahusiano mazuri na kituo
hicho cha Watoto Yatima cha Al-Madina, ambapo wamekuwa wakisaidia mara kwa
mara.
Mbali na msaada huo wa vyakula, vinywaji na sare za
shule na nguo, Multchoice-Tanzania pia imelipa pango la miezi sita la Kituo
hicho, ikiwa ni moja ya changamoto inayokisumbua sana kituo hicho chenye watoto
60.
Chande alisema kuwa wataendelea kukisaidia kituo
hicho pamoja na vingine ikiwa ni sehemu ya kusaidia jamii kupitia fedha
wanazopata kwa kuuza ving’amuzi bora kabisa vya DStv, ambavyo vimekuwa
vikinunuliwa kwa wingi.
Alisisitiza kuwa Multchoice-Tanzania itaendelea
kushirikiana na kituo hicho ili kuhakikisha watoto wanasonga mbele kwani ndio
taifa la kesho, ambapo kila mmoja wetu ana wajibu wa kujitolea kwa namna moja au
nyingine.
Hii sio mara ya kwanza kwa Multchoice-Tanzania
kukisaidia kituo hicho, kwani miezi kadhaa iliyopita wakati wa Mfungo wa Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani walikabidhi cherehanui kadhaa, ambazo zinatumiwa
kuendeleza kipato chao kwa kushona nguo na kuziuza.
Akitoa shukrani Mkuu wa Kituo hicho, Bi. Kuruthum
Yussuf alimshukuru Chande na Multchoice-Tanzania kwa ujumla kwa misaada
wanaokipatia kituo hicho kwa miaka mingi sasa.
Hatahivyo, Bi. Kuruthum alisema kituo chao
kinakabiliana na baadhi ya changamoto kama ukosefu wa eneo kwani kituo kipo
katika eneo dogo lililobanwa sana, ambalo linawafanya watoto washindwe kucheza
na kufanya shughuli zingine.
Aliwataka watu na taasisi mbalimbali kujitokeza
kusaidia kama wanavyofanya Multchoice, ambao wamekuwa wamkikisaidia kituo hicho
bila ya kuchoka.
Baada ya kumalizika kwa hafla ya kukabidhi msaada
huo, Chande alitembezwa katika kituo cha ushonaji, ambacho kiko meta chache
kutoka kilipo kituo hicho cha watoto yatima.
No comments:
Post a Comment