Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKATI mashindano ya taifa ya netiboli yanatazamiwa
kuanza Desemba 30 kwenye Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, mabingwa watetezi
Temeke wameutema ubingwa huo hata kabla ya kuingia dimbani kwa sababu ya ukata.
Mashindano hayo yanashirikisha timu za mikoa, huku Halimashauri
za Temeke, Ilala na Kindondo mkoani Dar es Salaam, kila moja ikipewa hadhi ya
mkoa katika mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka.
Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania, Chaneta,
Zainab Mbiro amesema leo kuwa mikoa ya Dodoma, Mwanza, Tabora, Shinyanga,
Manyara, Arusha, Mara, Morogoro, Simiyu na Singida imethibitisha kushiriki katika mashindano hayo.
Mbiro ambaye ni Mkuu wa Wilaya mstaafu alisema kuwa, Dar es Salaam akiwa na maana Halimashauri zake
zote tatu za Ilala, Temeke na Kinondoni, hakuna iliyothibitisha kushishiriki
katika mashindano hayo.
Katibu Mkuu wa timu ya Temeke, ambayo ndio bingwa
mtetezi, Amina Mussa amethibitisha leo kuwa, ukata umewafanya washindwe
kuthibitisha kushiriki mashindano hayo, licha yao kuwa mabingwa watetezi.
Temeke imelitwaa taji hilo kwa mara tatu mfululizo na
kama ingeshiriki mwaka huu na kulibeba, ingekuwa imelitwaa kwa mara ya nne
mfululizo.
Amina alisema kuwa pamoja na jitihada zao kupeleka
barua kwa mbunge wa Temeke, Meya na naibu Meya, lakini hadi sasa barua zao
hazijajibiwa lolote na wamepoteza matumaini ya kusaidiwa na watu hao.
Alisema kuwa Mbunge aliyepita wa Temeke, Zuberi
Mtemvu ndiye alikuwa mlezi wa timu hiyo na aliisaidia sana katika maandalizi
yake na kuhakikisha inafanya vizuri katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.
Alisema kuwa timu yao tangu Mtemvu ashindwe Ubunge imekuwa
ikitapatapa, ambapo ilishindwa kushiriki hata mashindani ya Ligi Daraja la
Kwanza yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro na hawajui hatma yao kama
watashushwa daraja kwani walishindwa hata kulipia ada.
“Viongozi hao tuliwaandikia barua ya kuwajulisha
kuhusu mashindano hayo ya Morogor, lakini hadii hii leo tunaongea na wewe
hakuna majibu na hatujui hatma yetu kama tutashushwa daraja au kufungiwa, “alisema
Amina na kungeza:
“Tangu Mtemvu atoke madarakani Temeke tumekuwa watu
wa kusuasua katika michezo, kwani
viongozi wetu wa sasa wako kimya kabisa hawajasema lolote.”
Amina aliwaomba wafadhili mbalimbali kujitokeza ili
kuisaidia timu hiyo ambayo bado inaendelea na mazoezi kila siku na wako tayari
kwa mashindano mbalimbali yatakayojitokeza.
No comments:
Post a Comment