Na Mwandishi Wetu Dodoma
SERIKALI imevitaka vyama na mashirikisho ya michezo
nchini kwenda ngazi za vitongoji kusaka vipaji na kuviendeleza ili kuendeleza
michezo nchini,.
Hayo yalisemwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma
mjini, Christina Mndeme wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Kamisheni
ya Wachezaji Tanzania (Kawata) katika hoteli ya Dodoma jana.
Wanariadha wazamani, Mwinga Mwanjala (kushoto),
Gidamis Shahana na Peter Mwita wakifuatilia mkutano wa Kawata mjini Dodoma leo.
|
Alisema wachezaji wenye vipaji wako ngazi ya
vitongoji, vijiji na hata mitaa, hivyo alivitaka vyama na mashirikisho ya
michezo kupiga hodi huko ili kusaka vipaji na kuviendeleza.
Akitolea mfano hilo alisema hata akina Filbert Bayi
na Gidamisi Shahanga vipaji vyao viligundulika huko vitongojini na kuendelezwa
hadi kuliletea sifa taifa kwa kutwaa ubingwa wa dunia kwa nyakati tofauti.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC),
Filbert Bayi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kawata leo.
|
Aidha, Mndeme alisema kuwa Serikali imeitaka amati ya
Olimpiki Tanzania (TOC) kuhamia Dodoma na iko tayari kuwapatia eneo kwa ajili
ya kujenga ofisi.
Mndeme alisema kuwa Makao Makuu yamehamia Dodoma na
tayari Waziri Mkuu yuko Dodoma, hivyo aliwataka TOC kuwasilisha maombi ya
kiwanja Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), na nakala ya barua hiyo
kumpatia yeye ili wapatiwe eneo la kujenga ofisi.
“TOC kama bado hamjawasilisha maombi ya eneo CDA basi
fanyeni hivyo haraka na nakala ya hiyo barua mnipatie mimi ili mpatiwe kiwanja
hicho na nyinyi mhamie Dodoma, “alisema Mndeme.
Akizungumzia kuhusu matumizi ya dawa za kuongeza
nguvu michezoni ambalo ni janga la dunia kwa sasa, Mndeme alisema kuwa lazima
yapigwe vita kwani yanaharibu wanamichezo na hayatakiwi kutumiwa hata kidogo.
Alisema matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni ni
hatari na yanatakiwa yapigwe vita kwa nguvu zote.
Pia mkuu huyo wa wilaya alivitaka vyama na
mashirikisho ya michezo kuwashirikisha wachezaji katika kamati zao za utendaji
ili wachezaji wawe na uwakilishi wao badala ya kusemewa kila kitu.
Awali akizunumza kabla ya mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa
TOC, Bayi alisema michezo kwa sasa ni ajira, ndiyo maana IOC imehamasisha Kamati
za Olimpiki kuunda Kamisheni za Wanamichezo ili watambuliwe kuwa sekta muhimu
ya maendeleo ya michezo katika Taifa letu.
“TOC inazidi kuviagiza na kushauri vyama/mashirikisho
ya michezo ambayo bado hayajaunda Kamisheni zao kufanya hivyo ili kuwapa
wanamichezo sauti ya kuchangia katika maendeleo ya michezo hasa kutetea haki
zao panapohitajika, “alisema Bayi.
Bayi aliongeza kuwa, TOC inaamini kwamba kukiwa na uwakilishi
wa wanamichezo katika vyama vya michezo na asasi za umma nchi yetu itakuwa
imepiga hatua katika kupiga vita matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu katika
michezo.
Kamisheni itaweza kuendeleza hoja ya kuwasaidia
wachezaji waliostaafu kucheza ili waweze kuishi maisha bora baada ya kustaafu
kucheza.
No comments:
Post a Comment