Thursday 1 December 2016

Jarufu na wengine wawili wachujwa uchaguzi mkuu kamati ya olimpiki Tanzania


Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi (kulia) akiwatambulisha wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya TOC.Kulia ni Abdallah Juma na Harrison Chaulo.

Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Uchaguzi ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) imetangaza majina yaliyopita katika mchujo, huku makamu wa rais Hassan Jarufu akikatwa, imeelezwa.

Kuchujwa kwa Jarufu kunatoa fursa ya kukaribia kukalia kiti cha nafasi hiyo kwa mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Henry Tandau, ambaye miaka minne iliyopita alishindwa na Jarufu katika uchaguzi uliofanyika Dodoma.

Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TOC, Harrison Chaulo (kulia) akisisitiza jambo alipozungumza na waandishi wa habari jana. Kushoto ni mjumbe wa kamati hiyo, Abdallah Juma walipozungumza na waandishi wa habari..
Uchaguzi Mkuu wa TOC mwaka huu pia utafanyika Dodoma Desemba 10, ikiwa ni siku mbili baada ya kupatikana kwa viongozi wa Kamisheni ya Wachezaji (Kawata) katika uchaguzi wao.

Tandau kabla ya uchaguzi uliopita alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chuo cha TOC, nafasi ambayo sasa inashikiliwa na Suleiman Jabir.
Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid (kulia), na Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.
Katibu wa kamati hiyo ya uchaguzi, Harrison Chaulo alisema jana kuwa, Jarufu amekatwa baada ya kushindwa kutokea katika usaili na fomu yake kujazwa na chama ambacho sio mwanachama wa TOC.

Chaulo aliwataja wengine waliokatwa kwa sababu mbalimbali ambao wana haki ya kukata rufaa kama hawajaridhika kuwa ni Lukelo Willilo na Abdulrahman Mohamed Hassan waliokuwa wakiwania ujumbe.

Aliwataja waliopitishwa ni Rais wa sasa wa TOC na katibu wake, Gulam Rashid na Filbert Bayi, Suleiman Mahmoud Jabir (Naibu Katibu Mkuu).

Wakati Mhazini ni Charles Nyange, mhazini msaidizi ni Juma Khamis Zaidy, wajumbe kutoka bara ni Irene Mwasanga, Muharam Mchume, Noorelain Shariff, Noel Kiunsi, Amina  Lyamaiga, Donath Massawe na Juliana Yassoda.

Wakati waliopitishwa Zanzibar kuwania ujumbe ni pamoja na Nassra Juma Mohammed, Mussa Abdul Rabi Fadhil, Suleiman Ame Khamis, Abdulhakim Cosmas Chasama, Ramadhan Zimbwe Omar, Said Ali Mansab, Sheha Mohamed Ali na Shukuru Abbas Nassor.

Waliopitishwa kwania nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji kupitia Olimpians ni pamoja na Samwel Mwera, Fabiano Joseph na Zakia Mrisho.

Wagombea kuanzia jana ruksa kuanza kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo huku rufaa wakiruhusiwa kukata kuanzia jana hadi Desemba 2 kwa wale ambao hawataridhika na kuenguliwa.

No comments:

Post a Comment