Monday 12 December 2016

Gulam, Bayi, Irine warejea kwa kishindo TOC, Tandau aukwaa umakamu wa Rais katika uchaguzi uliofanyika Dodoma hoteli



Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TOC, Noorelain Sharrif akipiga kura wakati wa uchaguzi huo mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC), imepata viongozi wake watakaoongoza kwa miaka minne hadi kiindi cha Olimpiki ya Tokyo 2020, baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Dodoma Hotel mjini hapa na kumalizika juzi usiku.

Katika uchauzi huo ulioendeshwa na kufanyika kwa utulivu mkubwa, ulishuhudia mkufunzi a Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Henry Tandau akitwaa umakamu wa rais huku mwanamichezo maarufu Juliana Yassoda akikosa nafasi katika ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TOC.

 Amina akipiga kura wakati wa uchaguzi wa TOC.
Akitangaza matokeo hayo juzi usiku, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uchaguzi, Wakili Llyod Nchunga, aliwataja walioshinda  nafasi tano za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka Bara na kura zao kwenye mabano kuwa ni Irene Mwasanga (50), Noorelain Sharrif (48), na Muharam Mchume (39).

Wengine ni Amina Lyamaiga (32), na Donath Massawe (30), huku walioshindwa ni Katibu wa zamani wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Noel Kiunsi (24), na Yassoda (21).
 
Kwa upande wa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji Zanzibar walishinda ni Kocha wa Timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’, Nasra Juma Mohamed (44), Katibu wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA), Suleiman Ame Khamis (42), na Mussa Abdulrabi Fadhi (37).

Wengine ni Ramadhan Zimbwe Omar (33), na Sheha Mohammed Ali (30), huku waliopigwa chini ni Said Ali Mansab (28), Mwenyekiti ZAAA Dk. Abdulhakim Cosmas Chasama (27), na Shukuru Abass Nassor (8).

Ramadhani Zimbwe (mbele) na Rais wa Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka wakipiga kura.
Kwa upande wa Wana Olimpiki, Mwanariadha wa kike, Zakia Mrisho alishinda kwa kura 49, Samuel Mwera kura 48 na Fabian Joseph kura 44.

Nafasi za juu ambazo zilikuwa na Mgombea mmoja mmoja, Gulam Rashid alipata kura za ndiyo 48 na mbili za hapana, Makamu wa Rais Henry Tandau kura za ndiyo 44,  tano zikimkataa na moja ikiharibika.

Katibu Mkuu, Filbert Bayi alitetea kwa kishindo nafasi yake hiyo baada ya kuata kura za ndiyo 49, huku hapana ni moja, Katibu Msaidizi Suleiman Mohamed Jabir akichomoza kwa kura 49 huku moja ikimkataa wakati Mweka Hazina ni Charles Nyange kura za ndiyo 47 huku hapana ni tatu na Mweka Hazina Msaidizi alichaguliwa Juma Khamis Zaidy kura 47, moja ikiharibika na hapana ni mbili.

Wapiga kura walikuwa 50, ambako uongozi huo utakaa madarakani kwa miaka minne.

Uchaguzi huo ulitanguliwa na ule wa Kamisheni ya Wachezaji (Kawata), mwishoni mwa wiki (Desemba 8), ambako Kassim Hussein Saleh alichaguliwa Mwenyekiti, Amina Lyamaiga Katibu huku Makame Ali Machano akichaguliwa kuwa Mjumbe TOC.

Wajumbe wawili kutoka Zanzibar ni Abdulrahaman Said na Tabia Maulid huku kwa upande wa Bara ni Patrick Nyembera na Magreth Eliud.

No comments:

Post a Comment