Mwandishi Wetu, Karatu
KLABU ya riadha ya Talent ya jijini Arusha jana
ilidhihirisha ukali wake baada ya wanariadha wake kushika nafasi za juu katika
mbio za kilometa 10 na zile za kilometa
tano katika Tamasha la 15 la Michezo na Utamaduni la Karatu.
Mgeni rasmi katika kilele cha tamasha hilo
kilichofanyika katika Uwanja wa Mazingira Bora mjini hapa alikuwa Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyekabidhi zawadi kwa baadhi
ya washindi.
Katika mbio za kilometa 10 kwa wanaume, Gabriel Geay
wa Talent alishinda kwa kutumia dakika 30:43.93 akifuatiwa na Fabian Joseph wa
Arusha dakika 30:48.11 nafasi ya tatu ikikienda kwa Josephat Joshua wa Polisi
aliyetumia dakika 30:55. 15.
Mshindi wa nne ni Bazil John aliyetumia dakika
31:12.51 wakati nafasi ya tano ikishikwa na Wilbard Peter dakika 31:40.70 wote
kutoka Polisi.
Kwa upande wa wanawake waliokimbia kilometa tano, Failuna
Abdi pia wa Klabu ya Talent alishinda akitumia dakika 17:01.49 akifuatiwa na
Magdalena Crispin naye wa Talent dakika 17:15.51, nafasi ya tatu ikaenda kwa
Jackline Sakilu wa JWTZ dakika 18:10.46.
Watoto waliokimbia kilometa 2.5 wasichana mshindi
aliibuka Elizabeth Boniface dakika 9:04.72 akifuatiwa na Rhoda Boniface dakika
9:26.84 wote kutoka Klabu ya Ligwa, huku nafasi ya tatu ikikamatwa na Rozalia
Kalole kutoka Mbulumbulu aliyetumia dakika 9:56.55.
Kwa upande wa mbio za Baiskeli kilometa 60 mshindi
aliibuka Richard Laizer aliyetumia saa 1:42.13 akifuatiwa na Gerald Didas saa
1:45.58 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Emmanuel Philemon 1:46.27 wote kutoka
Arusha.
Baiskeli wasichana mshindi aliibuka Annemarie
Griffioen saa 1:10.38 akifuatiwa na Habiba Mathias saa 1:25.40 huku nafasi ya
tatu ikinyakuliwa na Lore Desagner saa 1:26.55 wote kutoka Arusha.
Katika soka mabingwa waliibuka Karatu United baada ya
kuifunga Viwawa FC kwa mabao 3-0 huku washindi wa tatu wakiwa ni Nyuki FC na
nafasi ya nne ikatwaliwa na Laja FC.
Nape Nnauye, ambaye mbali na kuwapongeza waandaaji,
aliahidi kuanzia mwakani serikali itaanza kuingiza mkono wake katika kusaidia
uandaaji wa tamasha hilo.
Pia, alivitaka vyama mbalimbali vya michezo nchini,
kuiga mfano wa Karatu kwa kuandaa matamasha kama hayo ili kuibua na kuendeleza
vipaji.
Tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka, huandaliwa
na Filbert Bayi Foundation (FBF), na kudhaminiwa na Olympic Solidarity (OS),
kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).
No comments:
Post a Comment