Na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI wa Tanzania walioshiriki Michezo ya 31 ya
Olimpiki iliyofanyika Rio de Janeiro, Brazil wamerejea nchini na Jumapili
watafanyiwa tafrija nzito na kupewa zawadi na Kampuni ya Multchoive-Tanzania
kupitia DSTV.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki
Tanzania (TOC), Filbert Bayi, tafrija hiyo itafanyikia kwenye hoteli ya Serena
jijini Dar es Salaam.
Mbali na tafrija hiyo ambako pia watazawadiwa zawadi
nono kwa mujibu wa taarifa kutoka DSTV, wanariadha Alhamisi walikabidhiwa
zawadi za fedha taslimu kuanzia sh.500,000 hadi 200,000.
SABABU
YA ALPHONCE
Shamrashamra hizo zote tangu kuwapokea uwanja wa
kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA), ambako wanamichezo wengi
walijitokeza kuwalaki na baadae kukabidhiwa mashada ya maua na mabusu manono
kutoka kwa wake zao, zilitokana na nafasi ya tano iliyoshikwa na Alphonce Felix
katika mbio za marathoni.
Wake wa wanariadha, Alphonce Felix, Rehema (kushoto)
na yule wa Said Makula, Fatuma wakati wakisubiri kuwasili kwa waume zao kwenye
Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere (Jnia) Alhamisi.
|
Felix alimaliza mbio hizo katika nafasi hiyo kwa
kutumia saa 2:11:15 na kuhitimisha umwamba wa Juma Ikangaa wa kushika nafasi ya
juu kwa wanariadha wa Tanzania katika Michezo ya Olimpiki.
Ikangaa alimaliza wa sita katika Michezo ya Olimpiki
iliyofanyika Los Angeles, Marekani 1984 kwa kutumia saa 2:11:10 na hivyo kubaki
bado akishikilia rekodi ya kuwa mwanariadha wa Tanzania mwenye kasi zaidi katika
Michezo ya Olimpiki pamoja na Felix kumaliza katika nafasi ya juu kuliko
Ikangaa.
ZAWADI
ZA FEDHA TASLIMU
Felix kwenye Uwanja wa Taifa alizawadi kitita cha sh
500,000 huku wenzake Said Makula aliyemaliza katika nafasi ya 43 na Fabian
Joseph aliyeshika nafasi ya 112 pamoja na Sara Ramadhani ambaye hakuwepo siku
hiyo na kocha Francis John, kila mmoja aliondoka na sh 200,000.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka DSTV, kamapuni hiyo ya
king’amuzi cha michezo yote imeahidi kutoa zawadi nono siku hiyo mbali na
kuwaandalia chakula cha jioni wachezaji hao pamoja na viongozi wao.
Taarifa hiyo ilisema kuwa wachezaji hao wote saba,
wanne wa riadha, mmoja wa judo (Andrew Mlugu) na wawili wa kuogelea (Hilal
Hilal na Magdalena Moshi), wote watakabidhiwa zawadi hizo nono ambazo
zimeahidiwa na DSTV.
Mbali na zawadi zingine huenda DSTV wakampatia kila
mchezaji king’amuzi kilicholipiwa kwa ajili ya kufaidi uhondo wa kungalia
michezo yote duniani.
Kupokewa
kwa Shangwe
Wengi wanajiuliza sababu za Felix kupokewa kwa
shangwe wakati hakupata medali yoyote katika michezo hiyo ya Olimpiki.
Kaimu Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT),
Ombeni Zavalla `Avintishi’, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa
(BMT), Mohamed Kiganja na Katibu wa Kamati ya Ufundi ya RT, Rehema Killo.
|
Uongozi wa Riadha Tanzania (RT) pamoja na wadau
mbalimbali wa michezo wanasema kuwa mwanariadha huyo amefanya kile ambacho kwa
muda mrefu hakijafanywa na wanariadha wa Tanzania katika michezo hiyo mikubwa
kabisa duniani inayoshirikisha zaidi ya mchezo mmoja.
Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla alisema kuwa Felix
ameliondolea aibu taifa kwa kumaliza watano kwani kwa miaka mingi wanariadha wa
Tanzania hawajawahi kumaliza katika nafasi 10 za kwanza.
Ikangaa
anasemaje?
Ikangaa akizungumza katika mapokezi ya akina Simbu alisema
kuwa kuwa amefarijika sana kuona mwanariadha huyo chipukizi akimaliza katika
nafasi nzuri na hata kuipiku nafasi yake ya sita aliyoiweka mwaka 1984.
Anasema kuwa huu ni mwanzo mzuri baada ya miaka mingi
ya kushindwa kufanya vizuri katika michezo mikubwa kama hiyo.
Anasema kuwa siri ya mafanikio ni maandalizi ya muda
mrefu na kujali pia mchango wa wanariadha wakonge kama yeye ili kutoa uzoefu wao
katika mbio hizo na zingine.
Anakiri kuwa mbio za marathoni ni ngumu sana hasa
katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia kwani watu wamekuwa wajanja na
mbinu nyingi.
Kocha wa timu ya riadha ya Tanzania iliyoshiriki
Michezo ya 31 ya Olimpiki ya Rio 2016, Francis John (kulia) akiwa na Kaimu
Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja kwenye Uwanja wa ndege.
|
Kocha
wao anasemaje?
Kocha wa timu hiyo ya Tanzania, Francis John anasema
kuwa tangu awali wakati wa mazoezi aliahidi kurudi na medali kutoka katika
michezo hiyo, lakini ilibaki kido tu wamenusurika kupata medali.
Anasema kuwa kutokana na maandalizi na muda wa Felix
alijua mwanariadha wake huyo anaweza kufanya vizuri licha ya uchanga wake na
kushiriki mashindano machache ya kimataifa.
Anasema yeye ndio alimuhamisha Felix kutoka katika
mbio za meta 10,000 za uwanjani na kumuhamishia katika marathon baada ya kuona
kuwa mwanariadha huyo alishindwa kuboresha muda wake katika mbio hizo.
“Mimi ndio nilimuhamisha mbio Felix kutoka zile za
meta 10,000 za uwanjani na kumuhamishia marathon baada ya kuona alishindwa
kuboresha muda wake, “anasema Francis katika mahojiano hayo maalum baada ya
kurejea kutoka Brazil walikoshiriki Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016.
Kiongozi wa Msafara wa timu ya Tanzania iliyoshiriki
Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016, Suleiman Jabir mara baada ya kutua kwenye
Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere akiwa na mkewe.
Naye kiongozi wa msafara wa timu hiyo Suleiman Jabir anasema kuwa mashindano yalikuwa mazuri na Wabrazil walijiandaa vizuri ukilinganisha na uchumi wa nchi yao.
Jabir ameendelea kusisitiza kuwa wachezaji wetu waanze maandalizi mapema kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 ili tuweze kurudi na medali.
Wadau nao walifika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Dar es Salaam siku hiyo.
|
No comments:
Post a Comment