Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na
majonzi kifo cha msanii wa muziki wa taarab, Bi Shakila Said (pichani) kilichotokea ghafla
nyumbani kwao Mbagala jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo.
Katika taarifa ambayo imetumwa kwa vyombo vya habari na kusainiwa
na Katibu Mkuu BASATA, Geofrey Mwingereza, Shakila ni msanii na mdau
wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini na alikuwa na mchango mkubwa katika
kukuza muziki wa taarab nchini.
Pia taarifa hiyo ilisema Shakila alibuni kazi za sanaa za muziki
mbalimbali ambazo zilikuja kupata umaarufu mkubwa ambazo ni 'Macho Yanacheka'
na 'Kifo cha Mahaba'.
Mwingereza alisema mchango wake katika muziki wa taarab hasa
katika kubuni na kutunga nyimbo zenye ubora, ujumbe na maadili kwa jamii hautasahaulika
kamwe kwani ameacha misingi na alijitolea kwa kuufikisha muziki wa taarab
mahali ulipo leo.
"Baraza, wasanii na wadau wote wa sanaa hatuna budi kuendelea
kuenzi mema aliyotuachia marehemu Shakila na baraza linatoa pole kwa ndugu wa
marehemu, shirikisho la muziki, wasanii na wadau wote wa sanaa katika kipindi
hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu," alisema Mwingereza.
Bi Shakila Mwasisi wa taarab aliyesimama jukwaani kwa zaidi ya
miaka 40, alipitia katika makundi mbalimbali ya taarab yakiwemo ya Lucky Star, JKT na mengineyo.
Alijaliwa kupata watoto 13 na wajukuu zaidi ya 20.
Alistaafu muziki akiwa na JKT Taarab mwaka 2009, lakini amekuwa akiliimbia kundi hilo pale wanapomuhitaji na kumlipa posho.
Innalillah wainnah ilayh raajiuun
No comments:
Post a Comment