Sunday, 23 August 2015

Usain Bolt aendelea kutamba mbio za mita 100 duniani ashinda Beijing, China



Usain Bolt wa Jamaica akishangilia baada ya kushinda mbio za mita 100 katika mashindano ya dunia ya riadha yanayoendelea jijini Beijing China.
BEIJING, China
MWANARIADHA Usain Bolt alidhihirisha ubabe katika mbio za meta 100 baada ya kumshinda mpinzani wake Justin Gatlin kwa sekunde kadhaa na kufanikiwa kutetea ubingwa wake huo katika shindano la dunia la riadha jijini hapa.

Bolt alikimbia kwa kasi zaidi na kushinda mbio za nusu fainali na kuweka muda wake bora wa msimu kwa kutumia sekunde 9.79 na kushinda taji hilo kwa mara ya tatu.

Gatlin, 33, hajashindwa katika mbio 28 na alianza mbio za jana akipewa nafasi kubwa ya ushindi baada ya kukimbia kwa kutumia sekunde 9.77 katika mbio za nusu fainali. Lakini Bolt,mwenye umri wa miaka 29, alianza vizuri mbio za fainali na kushinda medali yake ya tisa ya dhahabu duniani.

Mmarekani Trayvon Bromwell na Mcanada Andre De Grasse wote walipata medali ya shaba baada ya wote kumaliza kwa kutumia sekunde 9.91.

No comments:

Post a Comment