Mahafali ya Shule ya awali Joyland yalivyofana Kigamboni
Na Mwandishi Wetu
WAZAZI wamehimizwa kujenga utamaduni wa kupitia kazi
na watoto wao wanaporudi shuleni kwa lengo la kusaidia ufahamu wao na
kuwarahisishia kazi walimu katika suala la taaluma.
Pia wamekumbushwa kufuatilia nyendo za watoto wao
kujua wanacheza wapi, na akina nani na rafiki gani wanaokuwa nao kwa muda mrefu
sambamba na kutowaachia kutumia muda mrefu kwenye runinga kwani ni moja ya
sababu ya kuharibika kwao na kuporomoka kimasomo wawapo likizoni.
Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Shule ya
Kimataifa ya Joyland, Fredrick Otieno wakati wa mahafali ya wanafunzi wa masomo
ya awali wa shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki shuleni hapo, Tua Ngoma,
Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Otieno alisema ushirikiano wa wazazi na walimu
katika malezi ya watoto ni msaada mkubwa wa wanafunzi, lakini kama wazazi na
walezi wataliacha jukumu hilo kwa walimu tu ni mtihani mkubwa na kuchangia
kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini. Alisema ni lazima wazazi na walezi
wakague madaftari na kazi za watoto wao wawapo majumbani na pia kuwazuia
kuingia katika makundi au kuumia muda mrefu kucheza wakati wa likizo ili
viwango vyao kitaaluma visiporomoke.
Pia aliwakumbusha wazazi na walezi kujenga tabia ya
kuwalipa ada watoto wao ili kurahisisha kazi kwa shule wanazosoma kuwa kile
kinachostahiki, alisema kucheleweshwa kwa ada ni tatizo ambalo linapunguza
morali wa kazi kwa walimu, ingawa alisema Joyland imekuwa ikijitahidi
kuhakikisha wanafunzi wanakipata kile kilichowapeleka wakati wazazi na walezi
wakikumbushwa wajibu wao wa kuwalipia ada.
Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa hakuna hazina bora
kama mtoto kupewa elimu ambayo huja kumsaidia ukubwani kwa kuzingatia kuwa
dunia ya sasa inaendeshwa kisasa na bila elimu bora na ya kutosha ni vigumu
kijana kusimama na kukabiliana na changamoto hizo.
Naye Mkaguzi Mkuu wa Elimu Kanda, Shani Kanungira
aliwasisitiza wazazi kutumia kujitolea na kutimiza wajibu wao kuwasomesha
watoto badala ya kutumia fedha nyingi kwa mambo yasiyo na tija kwa watoto na
familia zao kwa ujumla.
Shani alitoa nasaha yake kabla ya kumpisha
Mwakilishi wa Ofisa Elimu ya Msingi Manispaa ya Temeke, Frank Makingi
aliyesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kujenga utamaduni wa ushirikiano
dhidi ya walimu wa shule wanazosoma watoto wao.
Makingi alisema siyo kila jambo la wanafunzi kuachwa
mikononi mwa walimu tu, kadhalika alikumbusha kuwasaidia watoto katika kuwalea
katika maadili mema ili kulifanya taifa kuwa na raia wema na viongozi wazuri na
waadilifu wa baadaye.
No comments:
Post a Comment