RISALA FUPI YA KAMATI YA OLIMPIKI
TANZANIA WAKATI WA UFUNGUZI
Mhe. Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa
Pwani.
Mtaalamu wa Mafunzo-Ndugu Tuma.
Waratibu wa Mafunzo, TOC na AWATA,
Washiriki wa Mafunzo,
Waandishi wa Vyombo vya
Habari-Michezo
Mabibi na Mabwana.
Kwa niaba ya Kamati ya Olimpiki
Tanzania na kwa niaba yangu napenda kuupongeza uongozi wa Chama cha Mieleka
Tanzania (AWATA) kwa kufanikisha mafunzo haya kuanza kwa muda uliopangwa hali
kadhalika kufanikisha kwa ushirikiano na
Shirikisho la Mieleka la Dunia (UWW) kuwateua Wakufunzi wawili (2) Ndugu Pino
Massidda (Ufaransa) na Eric Ciacke (Cameroon)
ambaye atafika hapa tarehe 12/08/2015.
Mtaalamu Pino Massidda siyo mgeni
sana katika Bara la Afrika, amewahi kufundisha mafunzo kama haya katika nchi za
Afrika ya Magharibi hasa zinazozungumza
lugha ya Kifaransa kama Togo, Senegal, Ivory Coast n.k.
Chama cha Mieleka Tanzania (AWATA)
wakati huo ikishirikiana na Chama cha Mieleka cha Zanzibar (AWAZA) kwa mara ya
mwisho nakumbuka walipata mafunzo kama haya mwaka 2005 ambayo yalifanyika mjini
Morogoro kwa kushirikisha walimu 30
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Ni matumaini ya Kamati ya Olimpiki
Tanzania na Shirikisho la Mieleka la Kimataifa (UWW) walimu hao baada ya kufuzu mwaka 2005 bado
wanaendelea na fani ya ufundishaji katika Mikoa yao.
Siku za karibuni mchezo wa mieleka
umekuwa hausikiki sana. Taarifa nilizozipata ni kwamba viongozi waliotangulia
kabla ya huuambao uko madarakani waliutelekeza mcezo wa mieleka mpaka ukakosa
mwelekeo. Kamati ya Olimpiki Tanzania
kwa kuthamini mwelekeo mzuri wa viongozi walio madarakani imeona haina budi kuwapatia mafunzo haya ya
daraja la 1 ili wapatikane walimu wengi watakafundisha mieleka na kufikia hatua
ya kutuwakilisha Kimataifa.
Ndugu Mgeni Rasmi, mafunzo yanayogharimiwa
na Olimpiki Solidariti kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania ni ya gharama sana,
nashauri washiriki watakapomaliza mafunzo haya yanayoanza muda mfupi ujao wawe
na chachu ya kuuendeleza mchezo wa Mieleka katika vilabu na mikoa yao
wanayotoka.
Sina shaka AWATA tayari ina mipango
mahsusi kwa vijana hasa kwenye ngazi za shule. Ni wakati muafaka sasa AWATA ikawa
na wanamichezo wadogo katika ngazi mbalimbali kwa kufuata umri (chini ya miaka
15, 17, 20). Wanamichezo hao wakiandaliwa vizuri nina uhakika watafanya vizuri
katika siku za usoni.
Nawapongeza walimu washiriki katika
mafunzo haya. Ni matumaini yangu wote mliofanikiwa kuja hapa mmechaguliwa kwa
chama kuwathamini na watawategemea sana baada ya kumaliza mafunzo. Ninawaomba
muitendee haki nafasi hiI mliyopewa ya kuja hapa kuongeza ufahamu zaidi katika
masuala ya kufundisha mieleka pamoja na
kwamba wengi wenu bado mnacheza. Baada ya kuhitimu hapa na kila mmoja wenu akawa
na timu yake ya vijana, basi muda si mrefu tutakuwa na wachezi wengi.
Walimu tusitosheke na hapa
tutakapofikia, tujiendeleze zaidi kwani mambo mengi kuhusu ufundishaji mieleka yanabadilika
siku hadi hadi. Nina matumaini makubwa kwamba kuna siku mieleka itatuwakilisha
katika mashindano ya Kimataifa.
Chama cha Mieleka Tanzania irudi
kwenye njia yake baada ya kukosa mwelekeo kwa kuanza na kuandaa mashindano ya Vilabu na Taifa. Ni
muda mrefu mashabiki wenu wamekosa uhondo wa kuona mchezo wa mieleka.
Ninawaomba viongozi wa AWATA kwa
kushirikiana na baadhi ya wachezaji wa zamani wa AWAZA kufufua mchezo huu huko
Zanzibar na Pemba kwani ulishakufa na kutolewa katika orodha ya vyama wanachama
wa Kaamati ya Olimpiki Tanzania baada ya kutokuwa hai kwa muda mrefu.
Mwisho, ninaomba AWATA kuwawekea mazingira
mazuri walimu hawa kwa kuwatumia katika
mipango ya kuendeleza mchezo wa mieleka katika
ngazi mbalimbali nchini mwetu.
Ninaomba sasa nimkaribishe mgeni
rasmi aseme machache na atufungulie mafunzo haya, Karibu Mgeni Rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
RISALA YA MGENI RASMI WAKATI WA UFUNGUZI
WA MAFUNZO YA WALIMU WA MA MCHEZO WA MIELEKA, MKUZA, KIBAHA
10 AGUSTI, 2015.
Ndugu Filbert
Bayi, Meja Mstaafu na Katibu Mkuu, Kamati ya Olimpiki Tanzania,
Rais Chama cha Mieleka
Tanzania,
Katibu Mkuu,
Chama cha Mieleka Tanzania
Waratibu wa
Utawala (TOC) na Ufundi AWATA)
Wakufunzi wa
Mafunzo Pino Massidda (France) na Eric Ciake, (Camerou)
Viongozi wa
Mpira wa Wavu Mkoa wa Tanga,
Walimu Washiriki
wa Mafunzo,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na
Mabwana.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo. |
Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii
kuishukuru Kamati ya Olimpiki Tanzania kwa kunialika kuja kufungua mafunzo haya ya aina yake kufanyika kwa mara ya
kwanza hapa Kibaha, Mkoa wa Pwani. Nimefahamishwa haya ni mafunzo ya pili
kufanyika kwa ufadhili wa Olimpiki Solidariti na kuandaliwa kwa pamoja TOC na AWATA.
Nami kama
Kiongozi wa Serikali katika Mkoa huu
nawakaribisha katika manispaa yetu. Ni matumaini yangu kwa wanaotoka nje
ya Mkoa wa Pwani, wenyeji wenu wamewakaribisha katika Mkoa wetu.
Aidha pia niwapongeze TOC kuitikia ushauri wa Viongozi mbalimbali wa
Serikali ya Muungano la kutaka viongozi wa vyama na mashirikisho ya michezo
kuendeleza michezo katika Taifa letu ili kufikia viwango vya Kimataifa. Nami
kama Kiongozi wa Serikali katika Mkoa huu wa Pwani nawaunga mkono hao viongozi
na wapenzi wenye kiu ya maendeleo ya michezo. Tuwape elimu walimu ambao
watakuwa na uwezo wa kuwaandaa wachezaji katika ngazi ya Kimataifa.
Lengo hili
halitafanikiwa kama hatutakuwa na walimu wenye taaluma ya kuwandaa wanamichezo
kufikia azma hiyo.
Kamati ya
Olimpiki Tanzania na Chama cha Mieleka Tanzania hawakufanya kosa kuchagua Mkoa
wa Pwani hususani Kibaha kuwa mwenyeji wa Mafunzo haya
muhimu. Wananchi wa Pwani ni wakarimu na wapenda michezo ya aina mbalimbali.
Nawashukuru wote kwa kutupa heshima hii ya kuwa mwenyeji.
Ni heshima kubwa
kukutana na walimu mbalimbali kutoka Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar, hali
kadhalika na Wataalamu wa Shirikisho la Kimataifa la Mieleka (FILA) Nugu Pino
Massidda (France) na Eric Ciake (Cameroun).
Nawapongeza
walimu washiriki katika mafunzo haya. Ni matumaini yangu wote mliofanikiwa kuja
hapa mmechaguliwa kutokana na uwezo wenu katika ufahamu wa mchezo wa Mieleka
katika Mikoa yenu, kwa hiyo jitihada za ziada zinahitajika ili muweze kuongeza
ufahamu zaidi kutoka kwa wataalamu hawa wa Kimataifa ili baada ya mafunzo haya
muwe tofauti na mlivyoanza.
Ikiwa nchi yetu
itakuwa na walimu wengi wa mchezo wa Mieleka, na wakatawanywa kwenye shule zetu
ambapo ndiyo kwenye vipaji, basi miaka 5 ijayo tunaweza kuwa na uwakilishi
mzuri katika Michezo ya Kimataifa, lakini ikiwa walimu hawa watabaki kwenye
vilabu vya taasisi za Serikali (JWTZ,
Polisi, Magereza, Jeshi la Kujenga
Taifa, Jeshi la kujenga Uchumi nk.) ambazo nyingi ziko katika miji yetu
mikuu basi tutabaki pale pale tukitafuta mchawi
wa maendeleo ya mchezo wa mieleka. AWATA na AWAZA lazima wawe na mipango
mahususi ya kuendeleza vijana wa umri mbalimbali kuanzia kwenye shule zetu.
Serikali yetu ni
sikifu, mmeona wenyewe jinsi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Jakaya Mrisho Kikwete alivyo mstari wa mbele kuendeleza michezo hasa kwa
kuwalipa walimu wa nje wenye uwezo mkubwa kufundisha timu zetu za Taifa. Mhe.
Rais alianza kwenye Mpira wa Miguu, kila moja wetu anafahamu alipomleta Maximo (Brazil) kufundisha timu yetu ya
mpira wa miguu (Taifa Stars), Simmons
McKinns (Australia) kufundisha timu ya Netiboli (Taifa Queens) na kutoa
nafasi kwa Riadha Tanzania kumpata mwalimu kutoka nje, lakini mpaka leo
wamekuwa kimya bila kutekeleza ahadi aliyotoa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Tanzania.
Yote hayo ikiwa ni mchango wa Rais wetu.
Kwa hiyo AWATA/AWAZA
na walimu washiriki mnaohudhuria mafunzo haya kazi kwenu, elimu mtakayopata iwe
changamoto ya kunyanyua mchezo wa mieleka ili utupeleke kwenye ushiriki wa
Kimataifa na kutupatia heshima ambayo ndiyo kiu wa Watanzania.
Mwisho napenda
kuwashukuru Olimpiki Solidariti kwa kudhamini mafunzo haya, Shirikisho la Mchezo
wa Mieleka la Kimataifa (UWW) kuwaleta Wakufunzi wa Kimataifa, Kamati ya
Olimpiki Tanzania kwa ushirikiano na AWATA/AWAZA kuamua na kuandaa mafunzo haya
kufanyika katika Mkoa wetu wa Pwani, washiriki kwa kuhudhuria, kwani bila wao
tusingekuwa hapa leo.
Kwa haya
machache, sasa natamka kwamba Mafunzo ya Walimu wa Mchezo wa Mieleka
nimeyafungua rasmi.
Ahsanteni kwa
kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment