Waandishi Wetu
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limemuonya
mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, kuwa staili ya kampeni aliyoianzisha
ya kutembelea maeneo mbalimbali katika ziara zisizo rasmi, inahatarisha usalama
wa raia na mali zao, hivyo iachwe.
Onyo hilo limewagusa pia wagombea wa vyama vya siasa katika nafasi
mbalimbali hasa urais, ikielezwa kuwa, katika ziara hizo hujitokeza watu wengi,
ambapo pia wahalifu wanaweza kutumia mwanya huo kufanya vitendo vya uhalifu.
Akizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam,
Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova alisema, baadhi ya wagombea wa
vyama vya siasa wameanzisha mtindo wa kutembelea maeneo mbalimbali kama vituo
vya daladala na masoko kwa madai ya kuyatembelea makundi ya watu wenye kipato
cha chini.
Kamishna Kova alisema, kutokana na uzoefu uliojitokeza katika
ziara hizo zisizo rasmi, imeonekana mikusanyiko mikubwa isiyotegemewa katika
hali inayoashiria uvunjifu wa amani.
Kova alisema lengo la marufuku hiyo haliko kisiasa bali ni kwa
ajili ya usalama wa wananchi wote, kwani wao wanafanya kazi kwa mujibu wa
sheria na si siasa.
Alitaja miongoni mwa wagombea hao ni mgombea wa nafasi ya Urais
kupitia Chadema, Edward Lowassa pamoja na mgombea mwenza, Juma Duni Haji,
ambaye jana alikuwa akifanya ziara yake katika eneo la Kariakoo, wilaya ya
Ilala.
Alisema saa 6:00 mchana katika makutano ya mtaa wa Swahili na
Uhuru, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya alilazimika kukutana ana
kwa ana na Lowassa ili kumpa tahadhari ya kiusalama.
“Mgombea
huyo alikuwa amezungukwa na wapanda pikipiki wasiopungua 40 pamoja na magari
mengi, hali ambayo ilileta msongamano katika eneo hilo.
Lazima ieleweke wazi kwamba moja ya kazi za Jeshi la Polisi ni
kudhibiti makundi makubwa ya watu katika namna ambayo kiongozi yeyote wa aina
ya wagombea urais anatakiwa kulindwa katika kipindi chote cha kampeni hadi siku
ya uchaguzi,”
alisema Kova.
Alisema ni vyema wagombea mbalimbali hasa wa urais waoneshe
ushirikiano wa hali ya juu kwa Jeshi la Polisi ili kuzuia madhara yanayoweza
kujitokeza dhidi yao au kwa watu wengine.
Alisema jambo hilo linaweza kuonekana
ni kawaida lakini yakitokea madhara lawama zote zitaenda kwa polisi kwa kushindwa
kufanya kazi yao.
Hata hivyo, alisema marufuku hiyo ni kwa vyama vyote vyenye
wagombea wanaoshiriki katika uchaguzi mkuu na kwamba atakayeamua kukaidi agizo
hilo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Kamanda Kova alishauri viongozi wa vyama pamoja na wagombea
wao kufuata ratiba za kampeni za mgombea urais na mgombea mwenza kwa vyama vya
siasa kama ilivyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuondoa hisia za
kufanyika kampeni nje ya ratiba.
No comments:
Post a Comment